Na. Edward Kondela

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoa jicho la pekee katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kwa kuongeza mabwawa ya kunyweshea mifugo na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kulinda malisho.

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango amebainisha hayo leo (10.02.2024) Wilayani Longido akiwa kwenye ziara ya kikazi wakati akizindua Kituo cha Afya Ketumbeine na mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa kwanza unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Ameongeza kuwa mabwawa yanayoonesha udhaifu yakarabatiwe na hiyo ndiyo itakuwa zawadi kwa wakazi wa Wilaya ya Longido kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Ndugu zangu hawa ni wafugaji, mmeanza kazi vizuri lakini, ninawataka tena kutoa jicho la pekee kwa Wilaya ya Longido, kuongeza mabwawa ya kunyweshea mifugo yao na kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kulinda malisho na mabwawa yanayoonesha udhaifu yakarabatiwe.” Amesema Mhe. Dkt. Mpango

Mhe. Dkt. Mpango amebainisha hayo baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha Bw. Thomas Ole Sabaya kumueleza Makamu wa Rais kuwa wafugaji hawana kazi nyingine zaidi ya kufuga hivyo wanategemea sana maeneo yao kwa ajili ya kufuga na malisho.

Pia, ameiomba serikali iwasaidie kuweka utaratibu ukiwemo wa wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye maeneo yao ili kulinda maeneo ya malisho wakati wote hali itakayoondoa ufugaji wa kuhamahama na kusababisha migogoro maeneo mengine.

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti amesema wizara imeendelea kusogeza huduma mbalimbali kwa wafugaji wa Wilaya ya Longido ikiwa ni pamoja na kuchimba mabwawa makubwa kwa ajili ya kusambaza maji kwa mifugo pamoja na majosho.

Mhe. Mnyeti amefafanua kuwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/24 serikali imetenga Shilingi Milioni 46 kwa ajili ya kujenga majosho mawili katika vijiji vya jirani pamoja na josho kubwa ambalo tayari limezinduliwa mwaka jana.

Aidha, amesema kutokana na ukame katika baadhi ya maeneo serikali itahakikisha inaendelea kusogeza maji karibu kwa kushirikiana na Wizara ya Maji ili wafugaji waweze kupata maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo.

Pia, amesema wizara kwa sasa inaendelea kuhamasisha ujengaji wa mabwawa ya kufugia samaki na kuiasa jamii ya kimasai kula samaki kama ambavyo baadhi yao wameanza kula.

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa kwenye ziara ya kikazi katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha, ambapo aliambatana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango amezindua pia mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Longido Samia, utakaogharimu Shilingi Bilioni Tatu.

Share To:

Post A Comment: