NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt.Charles Mahera amezitaka Timu za Usimamizi wa Huduma za Afya za Mikoa na Halmashauri kusimamia nidhamu kwa watoa huduma za afya kwenye maeneo yao. 

Dkt. Mahera ametoa agizo hilo leo Machi 18, 2024 kwenye kikao kazi cha cha viongozi wa timu hizo kilicholenga kujadili hali ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kilichofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.

"Tunakwenda kwenye bima ya afya kwa wote sasa, na kama hatutakuwa na huduma nzuri katika vituo vyetu vya Serikali watu watatukimbia na kufuata huduma kwenye vituo binafsi, hivyo nendeni mkasimamie nidhamu kwa watumishi hususani kwa wauguzi kuacha lugha chafu kwa wagonjwa na kufanyakazi kwa mazoea."

Pia amewataka wataalamu ngazi ya Mkoa na Halmashauri kufanya kazi kwa pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa afya ngazi ya msingi ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza kujituma kwa hali ya juu na kufanya kazi kwa weledi. 

Aidha, Dkt. Mahera pia amewataka kuhakikisha wanatunza vifaa na vifaa tiba vilivyonunuliwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini kwani Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa hivyo.

Pia amewataka kuhakikisha wanasimamia matumizi ya mfumo wa GoTHoMIS  katika ukusanyaji wa mapato ya vituo ili kuzuia matumizi ya fedha mbichi na rushwa kwa baadhi ya watoa huduma.

Dkt. Mahera ameendelea kusisitiza ubora wa utoaji wahuduma ambapo watumishi wanahitajika zaidi kwa mgonjwa na kufanya kazi  kwa kufuata  miongozo.

Amewataka kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa miradi ya afya ili ikamilike kwa wakati na kupunguza hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG). 

"Kama mkiona eneo linachangamoto za ujenzi kutokana na unyevunyevu fanyeni makisio mapema na kuja na bajeti ya maeneo husika"

Share To:

Post A Comment: