Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Arusha imempongeza Bw. Nassoro Shemzigwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa umaridadi wake wa kusimamia na kuhakikisha jengo la Utawala linakamilika katika ubora unaotazamiwa.
Mhe. Loy Thomas Ole Sabaya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha kwa niaba ya Kamati hiyo amesema anampongeza Mkurugenzi kwani hali ya maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo unaridhisha sana.
“Ngorongoro tunayoiona leo ni tofauti na Ngorongoro ya miaka ya ile, Ngorongoro ya leo imebadilika, hata Mkuu wa Mkoa amethibitisha toka alipoingia Bw. Shemzigwa mambo yakaanza kwenda kasi”-amesema Mhe. Sabaya
Aidha Mhe. Ole Sabaya amendelea kumtakia kila lililo jema Bw. Shemzigwa pia aendelee kuchapa kazi.
” Nakutakia kila la kheri Mkurugenzi, ongeza spidi ibadilishe Ngorongoro. Hata nyie watumishi mnajionea wenyewe kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan”.
Hata hivyo naye Mkuu wa Mkoa Mhe. John V.K Mongella amempongeza Mkurugenzi kwa juhudi zake anazofanya katika kusimamia miradi yote ya maendeleo ndani ya Halmashauri yake ikiwemo jengo la Utawala kwani mwanzo jengo hilo lilienda kwa kusuasua ila toka alipofika tu mambo yakabadilika.
“Nampongeza Mkurugenzi sana, tokea amefika ameweka nguvu kubwa sana, maana tulimpa muda kufikia mwezi wa kwanza mwaka huu 2024 jengo lianze kutumika, kweli limeanza kutumika. Mkurugenzi kaja na timu yake na mambo yamebadilika hongera sana” amesema Mhe. Mongella
Bwana Nassoro Shemzigwa aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mwaka jana 2023 na mwezi Juni alianza rasmi kazi ya kuisimamia na kuiongoza Halmashauri katika hali ya uadilifu na sasa mambo yanakwenda barabara.
Ikumbukwe Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilion 2.7 za kitanzania kwaajili ya ujenzi wa jengo la utawala, jengo hilo lipo hatua za mwishoni kabisa na limeanza kutumika tangu mwezi januari 2023 mpaka sasa Watumishi wote wamekwisha hamia katika Ofisi za jengo hilo jipya la Utawala.
Post A Comment: