Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya Kampuni ya uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kampuni hiyo ijini Dar es salaam.

 KAMPUNI ya Uendelezaji wa Joto Ardhi Tanzania (TGDC) imetakiwa kuonesha matokeo chanya kwa kuzalisha umeme kwa kutumia rasilimali ya Jotoardhi ili kuunga Mkono Mpango wa Serikali wa kuwa na Nishati Safi na Endelevu.


Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wakati wa kikao na Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni hiyo pamoja na Menejimenti ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukutana na baadhi ya taasisi na kampuni zilizo chini ya Wizara ya Nishati kwa lengo la kuona utendaji kazi wa taasisi hizo.

Aidha ameieleza TGDC kuwa wabunifu na kutumia uwezo wao wote kuhakikisha kampuni hiyo inaanza kuzalisha umeme kwa kutumia rasilimali ya Jotoardhi kwa kuwa tayari baadhi ya maandalizi yameshafanyika katika maeneo ya vipaumbele.

"Kama ambavyo Serikali imejipambanua kuwa inatekeleza Mpango wa Nishati Safi na Endelevu, ni wakati wa TGDC sasa kuonesha uwezo wao katika kufanikisha hilo ili kutoa mchango mkubwa kwa Taifa, " amesema.

Ameongeza ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya na ya haraka zaidi ni vyema wakaongeza ubunifu, uthubutu, kushirikiana na kutoridhika na kila wanachofanya ili kupiga hatua mbele zaidi. Hali hiyo itaondoa changamoto ya umeme unayoikumba nchi kwa kuzingatia kuwa nishati ya Jotoardhi ni endelevu.

Amefafanua kuwa Watanzania wanataka kuona umeme unaozalishwa kutokana na Jotoardhi, hivyo TGDC ni wakati wao sasa kuonesha uwezo wa kuleta matokeo Chanya kwa Taifa."Tumieni ubunifu na uwezo wenu wote kuhakikisha kile mlichokikusudia kinafanikiwa...

"Na kuonekana kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyoelekeza kuwa uzalishaji wa umeme utaongezeka kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo Jotoardhi, vilevile kuunga mkono Mpango wa serikali wa kuwa Nishati Safi na Endelevu,” amesema Kapinga.

Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza TGDC kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kuhakikisha umeme unapatikana na pia amewataka kutumia vyema weledi na taaluma walio nayo kulinda Kampuni hiyo ili kupata matokeo ya haraka.

“TGDC lazima muonyeshe mchango wenu Nishati Safi na Endelevu ili nchi na dunia ione uwepo wenu na Serikali inataka matokeo hivyo mjikite katika hilo na watanzania wanaamini katika matokeo,” amesema Kapinga.

Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Athumani Mbuttuka, amewaeleza TGDC kuwa ofisi yake iko wazi wakati wote ili kupokea changamoto zozote zinazowakabili ili kuwasaidia na kuzitatua pale watakapoona wanakwama katika kutekeleza majukumu yako.

Sambamba na hilo amewataka kushirikiana, kuwa wabunifu na wenye uthubutu kuhakikisha kile walichokikusudia kinafanikiwa na watanzania wanapata umeme.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TGDC Profesa Shubi Kaijage na Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba wamemuakikishia Naibu Waziri Kapinga kuwa watashirikiana kwa pamoja kuhakikisha wanazalisha umeme wa Jotoardhi haraka iwezekanavyo.

Pia amesema wanaendelea kutoa elimu ya rasilimli ya hiyo kwa wadau mbalimbali ili wawe na uelewa mpana zaidi kuhusu mradi huo wa kimkakati.

Amesema kampuni hiyo ina miradi mitano ya kipaumbele ambayo ni ule wa Ziwa Ngozi unaotajiwa kuzalisha Megawati 70 lakini kwa kuanzia wataanza na Megawati 30. Mradi Mingine ni wa Kiejo- Mbaka mkoani Mbeya Megawati 60, Songwe mkoani Songwe Megawati 5 hadi 38, Luhoi mkoani Pwani Megawati 5 na Natroni mkoani Arusha Megawati 60.

Miradi yote hiyo iko katika hatua mbalimbali ambapo nguvu kubwa imeelekezwa katika Mradi wa Ngozi ambapo tayari mtambo wa kuchoronga visima vya Jotoardhi umepelekwa huko na hivi karibuni wataanza kazi ya uchorongaji.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) Mha. Mathew Mwangomba akieleza maendeleo ya kazi zinazofanywa na Kampuni hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga (Hayupo Pichani) iliyofanyika jijini  Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Prof. Shubi Kaijage akizungumza na wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania(TGDC) wakati wa ziara ya kikazi ya Judith Kapinga Iliyofanyika katika Ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athuman Mbuttuka akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Kampuni ya Uendeshaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) Wakati ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga (Hayupo pichani) alipotembelea Kampuni hiyo, jijini Dar es salaam.
Share To:

Post A Comment: