Waziri wa Fedha, Mhe Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba leo amezindua Ofisi ya Kanda ya Kaskazini ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha na mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima na wafugaji wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.


Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Nchemba aliishukuru TADB kwa kazi nzuri inayoendelea kufanya katika kuinua sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini, pamoja na sekta ya fedha kwa ujumla.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta hii, imeendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo ili kuinua Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja, kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ajira, kuchukua hatua za kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu, pamoja na kubainisha fursa za masoko za mazao hayo zilizoko ndani na nje ya nchi yetu,” alisema.

Aliongeza kuwa ofisi hiyo ya Kanda ya Kaskazini ya TADB itakwenda kuimarisha huduma za kifedha kwenye Mikoa ya Kaskazini na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, wavuvi na wafugaji, kufungua fursa na kuendeleza zaidi ukuaji wa biashara katika mnyororo wa thamani katika mikoa yote minne ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga. 

Mikoa hiyo inasifika kwa kuzalisha mazao muhimu kwa uchumi wa nchi, kama vile kahawa, mahindi, ngano, na sekta zingine kama utengenezaji wa mbolea, ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa, ufugaji wa samaki na kuku wa nyama na mayai, kilimo cha maua, mboga mboga na matunda .


“Naihakikishia Bodi na Menejimenti ya TADB kuhusu utekelezaji wa agizo nililotoa wakati wa Bunge la Bajeti, ambapo nilitangaza kwamba Serikali itaiongezea Benki ya TADB na TIB jumla ya mtaji wa Shilingi Bilioni 235.9 kwa lengo la kupanua wigo wa mikopo kwa sekta binafsi kwa ajili ya miradi ya kukuza sekta za uzalishaji na kuongeza thamani.

Pia serikali itatekeleza programu ya kuwezesha mtaji usiopungua Shilingi Trilioni 1 kwa miaka mitano hadi kumi kwa benki kama TADB ili ziweze kufanya shughuli ya utoaji wa mikopo kwa ufanisi zaidi, na wakulima wazidi kupata mitaji ya kujiendeleza,” Waziri alisema.

Aliwasisitizia Wananchi wa mikoa hiyo kuchangamkia fursa ya uwepo wa Ofisi hiyo ya Kanda kupata uelewa zaidi wa utaratibu wa kupata mikopo, kufanya matumizi sahihi ya mikopo na kulipa kwa wakati, na pia kuishauri Menejimenti ya Benki na watumishi wake kuweka masharti nafuu ya mikopo, kuwatembelea wanufaika katika miradi yao na kutoa elimu ili kusimamia kikamilifu mikopo husika kwa wakulima, wavuvi na wafugaji.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw Frank Nyabundege alielezea kuwa ufunguzi wa ofisi hiyo ni mwendelezo wa mafanikio ya benki ya TADB kutimiza malengo yake kutoa mikopo ya masharti nafuu, kwa viwango vya riba za chini na kutoa muda mrefu zaidi wa marejesho kwa wakulima wadogo, wa-kati na wakubwa katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya kilimo, ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

“Hadi kufikia Novemba mwaka huu mizania yetu ya mikopo imeendelea kukukua na kufikia kiasi cha Shilingi Bilioni 600.7 mwezi Novemba, 2023. Ofisi hii ya Kanda ya Kaskazini inaenda kupunguza adha kwa kufikisha huduma za benki karibu zaidi na wateja wake waliokuwa wanahudumiwa na ofisi ya Dodoma, ambapo hadi kufikia Novemba 2023, TADB imekwisha wezesha wakulima na wafugaji wa kanda ya Kaskazini kwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 18.3 kwa Mkoa wa Tanga, Shilingi bilioni 7.9 Mkoa wa Arusha, Shilingi bilioni 3.2 Mkoa wa Kilimanjaro na Shilingi bilioni 3.1 kwa mkoa wa Manyara.

Mikopo hii imewezesha upatikanaji wa pembejeo na viwatilifu, mbegu bora za mifugo, ukuzaji viumbe hai kwenye maji na uvuvi.”

Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchochea maendeleo ya nchi kupitia kilimo na kuiongezea TADB mtaji wake kufika Shilingi Bilioni 268, pamoja na juhudi nyingine za kuongeza mitaji na mikopo ya masharti nafuu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.Tunathamini juhudi mbalimbali za serikali kuhakikisha benki yetu inafanya kazi kwa mafanikio ya malengo yaliyokusudiwa,” alisema.

TADB sasa ina ofisi saba mbazo ni Kanda ya Ziwa yenye ofisi Mwanza - na kuhudumia mikoa ya Kagera, Mara, Shinyanga, Geita na Simiyu; Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye ofisi Mbeya - na kuhudumia mikoa ya Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa.


Kanda ya Mashariki yenye ofisi Dar es salaam na kuhudumia mikoa ya Pwani na Morogoro; Kanda ya Magharibi yenye ofisi Tabora na kuhudumia mikoa ya Katavi na Kigoma; Kanda ya Kati yenye ofisi Dodoma na kuhudumia mkoa wa Singida; Kanda ya Kusini yenye ofisi Mtwara na kuhudumia mikoa ya Lindi na Ruvuma; na sasa Kanda ya Kaskazini yenye ofisi Arusha na kuhudumia Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.

“Aidha, tumeshapata ofisi ndogo Zanzibar tukiwa tunasubiri vibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kufungua ofisi kubwa na ya kisasa Zanzibar,” Bw Nyabundege alielezea.

Serikali iliamua kuanzisha Benki ya TADB mwaka 2015 kwa malengo makubwa mawili; Ambayo ni: kuchangia utoshelevu na usalama wa chakula nchini; pamoja na kuchagiza mapinduzi ya kilimo toka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara.


Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa ofisi za kanda ya Kaskazini za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) jijini Arusha Arusha. Ofisi hiyo ya kanda itahudumia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.





Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba (wa kwanza kulia) akizundua rasmi ofisi ya kanda ya Kaskazini ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) itakayohudumia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga. Wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni mmbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo akifuatiwa na mwenyekiti wa bodi ya TADB Ishmael Kasekwa.


Mwenyekiti wa bodi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Ishmael Kasekwa (kati kati) Akimtambulisha mkurugenzi mtendaji wa Benki hiyo Frank Nyabundege (kulia) kwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba (kushoto) muda mfupi kabla ya uzinduzi wa ofisi za kanda ya Kaskazini za benki hiyo uliofanyika jijini Arusha










Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba (kati kati) akisalimiana na wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi tawi la benki hiyo kanda ya Kaskazini jijini Arusha. Ofishi hiyo ya kanda itahudumia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.


Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akisalimiana na kufurahia jambo na Meneja Masoko na mwasiliano wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Amani Nkurlu (kulia) muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi tawi la benki hiyo kanda ya Kaskazini jijini Arusha. Ofisi hiyo ya kanda itahudumia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.

Share To:

Post A Comment: