Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb)  amekielekeza Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kujikita katika kutoa mafunzo yenye weledi, ubora na viwango vya hali ya juu ili kuendana na hadhi ya utoaji huduma kwa watalii kimataifa.

Ameyasema hayo Desemba 14,2023 alipofanya ziara ya kikazi katika Chuo cha Taifa cha Utalii kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu yake pamoja kuzipatia ufumbuzi changamoto walizonazo.

“Tumeendelea kuwasisitiza kuhusiana na dhamana ambayo wamepewa na Serikali katika kuandaa wahitimu wenye weledi, ubora na viwango vya hali ya juu ili watakapoenda huko wakatoe  huduma kwenye  Sekta ya Utalii pamoja na maeneo ya uratibu wa matukio inayoakisi taswira ya Taifa letu” Mhe. Kairuki amesema

Aidha, Mhe. Kairuki amesisitiza juu ya suala la kuwaandaa vyema wakufunzi wa chuo hicho katika masuala ya kitaalamu ya ukarimu, utalii, TEHAMA, kujiamini pamoja na kuwa na uwezo wa kumudu   lugha zaidi ya moja ili wawe na ushindani  katika soko la ajira kitaifa na kimataifa.

Katika hatua nyingine Mhe. Kairuki  ameitaka menejimenti ya chuo hicho kutafuta fursa mbalimbali na kushirikiana na vyuo vingine vya utalii vya nje ya nchi kama Kenya, Ufaransa, Marekani na Canada ili kuendelea kujifunza kutoka kwao.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo Mhe. Kairuki amesema kwa kuwa chuo hicho kina Kampasi mbalimbali jijini Arusha, Mwanza na Dar es Salaam kiangalie namna ya kuweza kudahili wanafunzi wengi zaidi na kukidhi  idadi na kiu ya kupata wataalamu ambao waajiri wangependa kuwapata.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara za Waziri Kairuki  za kujifunza namna Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zinavyofanya kazi na kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.

Share To:

Post A Comment: