Na Dotto
Mwaibale, Singida
WANANCHI wa
Manispaa ya Singida wameipongeza Taasisi ya MO Dewji Foundation na Shirika lisilo la
Kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL)
linalojishughulisha na kubadili maisha ya jamii baada ya kufufua visima 19 vya maji safi na salama vilivyo jengwa na Mohammed
Dewji wakati alipokuwa Mbunge wa Jimbo la Singida mjini.
Wananchi waliotoa
pongezi hizo ni kutoka katika kata ya Unyambwa, Unyianga, Mtamaa na Unyamikumbi
ambazo zipo katika Manispaa ya Singida.
Akizungumza
wakati wa zoezi la ufufuaji wa visima hivyo lililofanyika Novemba 2, 2023
katika kata hizo na kupata maoni ya wananchi , Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo
ambalo linasimamia ufufuaji wa visima hivyo , Joshua Ntandu alisema jumla ya
Sh. Milioni 119 zimetumika kufanya kazi hiyo.
“Lengo letu
lilikuwa ni kuona kama visima vilivyochimbwa awali je vinaweza kufanya kazi na
ndipo tuone kama kutakuwa na uhitaji mkubwa wa maji na ninyi sasa mje na
mapendekezo ya visima hivyo vichimbwe maeneo gani na vitatumia nishati ipi kwa
ajili ya kuyasukuma kama ni umeme wa jua au wa Tanesco na njia nyingine,”
alisema Ntandu.
Alisema mpango wa
ufufuaji wa visima hivyo ulikuwa ni wa muda mfupi lakini lengo lao ni kutaka
kuona mkoa mzima wa Singida unapata maji safi na salama na yapatikane umbali
usiozidi mita 400 kuanzia watu walipo.
Ntandu alihimiza
umuhimu wa kuvitunza visima hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu na
kutengeneza mpango mzuri utakaotumika kuvifanyia matengenezo vitakapokuwa na
changamoto ya kuharibika kwa kuwa wao hawatahusika tena na matengenezo hayo.
Mhandisi wa Maji
wa Shirika hilo, Edward Barnaba alisema baada ya kufanya upembuzi yakinifu wa
visima vyote 38 vilivyo chimbwa na Dewji
ni visima hivyo 19 pekee ndivyo vilivyoonekana kuwa vinaweza kufufuliwa na
kurudi katika hali yake ya kawaida ambavyo vitakamilika mapema mwezi huu wa
Novemba.
Barnaba alisema
visima hivyo vinaharibika kutokana na kuingia kwa mchanga na watoto kuweka mawe
kwenye pampu ya kusukuma maji na kuharibu mfumo wake ambapo alishauri jirani na
maeneo vilipochimbwa iachwe nafasi ya mita 60 na kuzungushiwa uzio ili
mazingira yake yasiharibiwe.
Kwa upande wake
Fundi Sanifu Mkuu Ubora wa Maji, Maabara ya Singida, Shifaya Munisi alisema
baada ya kupima ubora wa maji baada ya kufufuliwa kwa visima hivyo yameonekana
kuwa ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Mwakilishi wa Mo
Dewji katika ufufuaji wa visima hivyo , Janeth Mashauri, aliwataka wananchi ambao
visima vyao vimefufuliwa wavitunze kwani ni mali yao.
“Mo Dewji kazi
aliyoifanya ni kuvifufua visima hivi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ombi
langu kwao ni wavitunze na kurekebisha miundombinu yake itakapo haribika,”
alisema Mashauri.
Mkazi wa Kitongoji
cha Sanga Kata ya Unyambwa, Mwajuma Mohamed alizishukuru taasisi hizo kwa kufufua
visima hivyo na kueleza kuwa licha ya kufufuliwa bado kunachangamoto ya
upatikanaji wa maji hasa kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa kitongoji hicho
ambapo aliomba kama utakuwepo uwekano wachimbiwe visima vingine.
“Tunachangamoto
kubwa ya maji tunatoka saa tisa usiku kuja hapa kufuata maji na tunahatarisha
maisha yetu kwa kushambuliwa na fisi ni kweli maji tunapata lakini
hayatutoshelezi kwani wakati kinachimbwa kisima hiki watu walikuwa wachache
wasiozidi 200 lakini leo tupo zaidi ya 1500,” alisema Mwajuma.
Wananchi wengine
waliozishukuru taasisi hizo kwa kufufua visima hivyo na kuomba visima zaidi
viongezwe ili kusaidia kuondokana na
adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji ni Anifa Mkotya, Rehema Nasoro na
Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Sanga, Ongoza Samwaja.
Diwani wa Kata ya
Unyambwa, Shabani Magwe, Diwani wa Kata ya Mtamaa, Gwae Mbua, Diwani wa Kata
ya Unyianga, Geofrey Mdama na Diwani wa Kata ya Unyamikumbi, Kipandwa Ipini
wakizungumza kwa nyakati tofauti walizishukuru taasisi hizo kwa kuwakomboa
wananchi na kuwaondolea adha ya kupata maji.
Madiwani hao waliziomba taasisi hizo ikiwezekana ziwachimbie visima vingine ili kukabiliana na changamoto ya maji kutokana na ongezeko la watu kwani wakati visima hivyo vilipokuwa vinachimbwa mwaka 2008 na sasa ni miaka 13 imepita katika maeneo yao kulikuwa na watu wachache.
Diwani wa Kata ya Unyamikumbi, Kipandwa Ipini, akizungumzia visima hivyo. |
Wanawake wakichota maji katika Kisima kilichofufuliwa eneo la Sanga Kata ya Unyambwa. |
Wananchi wa Kitongoji cha Ntunduu Kata ya Unyamikumbi wakiangalia maji yaliyokuwa yakitoka katika kisima kilichofufuliwa eneo hilo. |
Watoto wakishuhudia maji yakitoka katika eneo hilo la Ntunduu. |
Post A Comment: