Na.Samwel Mtuwa- Dodoma.

Tanzania imefungua milango ya uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa nchi ya Korea ya Kusini ikiwemo  kuendeleza ushirikiano wa kikazi katika kufanikisha utekelezaji wa mikakati ya Vision 2030:MadinI Maisha na  Utajiri.

Hayo yamesemwa leo Novemba 8, 2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati wa mazungumzo ya ushirikiano wa kisekta baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa Korea Kusini yaliyofanyika jijini Dodoma. 

Wakati akizungumza na ujumbe huo kuhusu uwepo wa madini , Waziri Mavunde amesema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini mkakati kama vile madini ya kinywe, lithium , Nibioum na Makaa ya mawe ambayo kwasasa mataifa mengi yanatafuta kuwekeza huko kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na  maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Waziri Mavunde amezikaribisha kampuni mbalimbali  kutoka Korea ya Kusini kuja kuwekeza Tanzani na kuwaeleza  kuwa kwasasa sekta ya madini nchini Tanzania  ipo na vision2030 ambayo lengo lake ni kupata taarifa za utafiti ambazo zitatoa dira ya uwekezaji na uendelezaji kwa  kufungamanisha sekta za kiuchumi.

Akielezea kuhusu kufungua kiwanda cha uchakataji madini ya kinywe na uongezaji thamani madini nchini Tanzania , Mkurugenzi wa Kampuni ya POSCO ya nchini Korea Ji Ki Chun amesema , baada ya kukamilisha uchimbaji wa madini ya kinywe wilayani Mahenge watafungua kiwanda cha kuchakata madini ghafi ya Kinywe na uingezaji thamani  kabla ya kusafirisha nje ya nchi.

Chun amefafanua kuwa menejimenti ya POSCO imeridhika na hali ya  miundombinu nchini ikiwemo reli  ya kati pamoja ujenzi wa SGR.

Naye , Balozi wa Korea ya Kusini nchini Tanzania Kim Sumpyo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuimarisha uhusiano mzuri wa kiuchumi na serikali ya Korea Kusini amebainisha kuwa Korea Kusini ina mkataba wa hiyari katika ushirikiano wa kikazi ndani ya sekta ya madini hivyo itaendelea kutoa ushirikiano katika uwekezaji.

Balozi Sumpyo ameongeza kuwa mazingira salama na Sera nzuri  zinavutia wawekezaji wetu na kuahidi kuendelea kuwaleta wawekezaji wengi kutoka nchini korea kusini kuja kuwekeza Tanzania. 

Awali , akifungua mazungumzo hayo ya ushirikiano Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali ameimshukuru Balozi wa Korea kusini nchini Tanzania kwa uwekezaji mzuri katika sekta ya madini akitolea mfano uwekezaji katika madini ya Kinywe wilayani Mahenge.

Mahimbali amemuomba Balozi Sumpyo kuendeleza ushirikiana na kubadilishana  uzoefu wa kisekta baina ya wataalam wa Korea kusini na wataalam wa sekta ya madini Tanzania.


VISION2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI

Share To:

Post A Comment: