Na Yese Tunuka.


Moshi.JESHI  la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Semeni Feruzi Alfani  (45) Mkazi wa kitongoji Cha Reli Juu Wilaya ya Mwanga kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mwanaye wa kumzaa aitwaye Shamsidini Jamadu Msemo (13) kwa kumchoma moto.


Akizungumzia tukio Hilo kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro,Simon Maigwa amesema kuwa lilitokea Agosti 3,mwaka huu nyumbani kwa mtuhumiwa ambapo mtuhumiwa alimmwagia mafuta ya taa mwanaye huyo na kumchoma moto huku akiwa amemfunga kamba na kumsababishia majeraha makubwa yaliyopelekea kifo chake wakati anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.


Kamanda Maigwa amesema kuwa mtuhumiwa alitekeleza tukio hilo kwa kumtuhumu Marehemu kuwa alichukuwa viazi vya chipsi bila ruhusa ya mama yake na fedha kiasi Cha sh. 20,000/= .


"Baada ya juhudi za muda mrefu kwa kushirikiana na wananchi wema tumefanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo huko Ifakara mkoani Morogoro alipokuwa amekumbilia kwenda kujificha," amesema Maigwa.


Wakati huohuo Jeshi la Polisi  linamshikilia mtuhumiwa mwingine ambaye Jina lake limehifadhiwa kwa Sababu za kiuchunguzi kwa tuhuma za kusababisha kicho Cha Binti aitwaye Zuwena Bitariloho Bihumo (14) ambaye ni mfanyakazi wa ndani mwenyeji wa Kigoma.


Amesema kuwa tukio hilo lilitokea Octoba 23,mwaka huu Kijiji Cha Uswaa Wilaya ya Hai Kilimanjaro ambapo mtuhumiwa na mke wake walimfanyia ukatili kwa kumchapa na kitu kilichodhaniwa kuwa ni fimbo maeneo mbalimbali ya mwili wake na kupelekea majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake.


Amesema watuhumiwa baada ya kutenda ukatili huo walimpeleka binti huyo Hospitali ya Wilaya ya Hai kama mgonjwa huku wakitambua kuwa alikwisha fariki tayari.


"Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kiuchunguzi kukamilika " amesema Maigwa


Aidha Kamanda Maigwa ametoa Rai kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na wazazi kwamba Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vyovyote vya kikatili dhidi ya watoto huku akisisitiza kuwa Kilimanjaro bila ukatili wa watoto inawezekana.


Mwisho.

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: