Na Moses Ng'wat, Mbozi.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Dk. Fransis Michael amefanikiwa kumaliza mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Nanyala na  kiwanda cha Saruji Mbeya (MCC) kwa kuwezesha pande hizo mbili kila mmoja kupata hati za kumiliki maeneo yao kwa mujibu wa sheria.

Mgogoro huo uliodumu kwa miaka 19  katika Kijiji  hicho cha Nanyala, Wilayani Mbozi, umefikia tamati baada ya mwekezaji huyo wa kiwanda cha Saruji Mbeya (MCC) kukubali kuachia ekari 62.5 ambazo zimereshwa kwa serikali ya kijiji kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini ya chokaa, huku kiwanda hicho kikibaki na eneo la hekta 900.5.

Akiongea na wananchi baada ya kukabidhi hati hizo, Dk. Michael alisema kuwa Suluhu ya mgogoro huo imefikiwa baada ya vikao vya pamoja  kati ya serikali ya Mkoa, Kijiji cha Nanyala na kampuni hiyo ya Saruji Mbeya.

Dk. Michael alisema kuwa eneo walilokabidhiwa wananchi  ambalo ni ekari 62.5  ni kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa chokaa kwa  wachimabaji wadogo pekee, huku eneo lingine la kijiji likiendelea na matumizi ya awali ikiwemo kilimo na ufugaji.

Aidha, Mkuu wa Mkoa  Dk. Michael alisema kwa upande wa mwekezaji ambaye ni kiwanda cha Saruji Mbeya ambaye alikuwa akilimiliki eneo hilo kwa mujibu wa sheria tangu mwaka  1978 kwa sasa amebakiwa na hekta 905 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uchimabaji.

Hata hivyo, ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuendelea kuwapatia wananchi eneo hilo kwa njia ya mkataba wa mwaka mmoja mmoja au miwili ili waendele na shughuli za kilimo hadi hapo kampuni hiyo itakapoanza shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa Dk. Michael ameuataka uongozi wa kiwanda hicho kulipa kijiji hicho na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Mwakilishi wa kiwanda cha Saruji Mbeya, Ester Kuja ambaye ni mwanasheria wa kampuni akizungumzia suala hilo la Uwajibikaji kwa Jamii alisema kuwa kiwanda hicho hutoa fedha hizo katika Mkoa wa Mbeya kwa kuwa kiwanda kiko mkoani humo licha ya kwamba malighafi zinatoka mkoa wa Songwe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Nanyala, Yohana Mwambunga,  akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake, alisema kuwa mgogoro huo ulikuwa kero kubwa kwani ulileta sintofahamu kati ya serikali na wananchi kwa kuwa lawama zilikuwa zikielekezwa kwa serikaliy huku akimshukuru Rasi Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi huo.

Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho cha Nanyala,  Tamali Njela, alisema licha ya kupokea hati hiyo serikali ya kijiji ijitahidi kuwaonyesha wananchi mipaka yao ili kuepuka mgogoro mingine isiyokuwa ya lazima kati ya uongozi wa kiwanda na wananchi hao.

Mgogoro huo wa ardhi katika eneo hilo la kijiji cha Nanyala unahusisha ekari 2315 na umedumu kwa muda mrefu na kusababisha shughuli za maendeleo kukwama, huku wananchi wakiishi kwa hofu.

Mwekezaji huyo alimilikishwa kisheria eneo hilo na serikali, wakati huo Kijiji cha Nanyala kilichopo Wilaya ya Mbozi kikiwa ni sehemu ya Mkoa wa Mbeya kabla ya kugawanywa na kuangukia mkoa mpya wa Songwe na ameendelea kulitumia kwa ajili ya malighafi ya kiwanda chake kilichopo Mkoani Mbeya.


Mwaka 2017 baada ya mwekezaji huyo kutaka kupanua shughuli zake za uwekezaji,  alikumbana na upinzani kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho wanaodaiwa kulivamia eneo hilo la mwekezaji huyo aliyemilikishwa  na serikali .

Mwaka 2019 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt John Pombe Magufuli aliagiza Wizara za Ardhi, Madini, Tamisemi na Viwanda zishughulikie mgogoro wa Ardhi baina ya Kijiji cha Nanyala na kiwanda cha Saruji cha Mbeya.

mwisho.
 

Share To:

ASHRACK

Post A Comment: