Na Immanuel Msumba; Monduli

Wakazi wa Kata nne za Monduli mjini, Lashaine, Engutoto na Meserani Wilayani Monduli, Mkoani Arusha wameiomba serikali kuwafikishia huduma ya maji safi katika maeneo baada ya kukosa maji kwa zaidi ya miezi mitatu, tangu mwishoni mwa mwezi wa saba.

Mwandishi wetu alifika eneo hilo na kuzungumza na Bi Kalista Faustinemkazi wa Kitongoji cha Sinoni Kusini ambapo ametueleza kuwa toka mwezi wa saba mwaka huu hawajawahi kupata maji safi katika maeneo yao. Wajumbe wa nyumba kumi waliwapa taarifa kuwa pampu ya maji imeharibika na kwamba itapelekea kukosa maji kwa kipindi kifupi, ila mpaka sasa ambapo ni Miezi mitatu baadaye, bado hawana maji na wanaendelea kuteseka.

Tulizungumza pia na Bi Elizabeth Joshua ambaye ni mwalimu mstaafu na mkazi wa kata ya Monduli Mjini. Nae alitueleza kuwa katika mtaa wake maji hayajatoka kwa muda wa miezi mitatu na kuwapelekea yeye na familia yake kushindwa kufanya mahitaji yao ya kila siku kama kuoga, kufua na kuosha vyombo wanavyotumia.

“Mimi natoka ku puu nje ya nyumba yangu (kujisaidia) natumia karatasi kujifutiachoo changu kinanuka ndani, naiomba serikali ya Rais Samia itutue ndoo kichwani kama tunavyoona huko kwenye tv kwenye mikoa ya wenzetu" alisema.

Kwa upande wake Bw.Thomas Laizer Mjumbe wa nyumba kumi katika mtaa wa Kitongoji cha Sinoni Kusini amekiri kukosekana kwa maji kwa miezi yote mitatu katika eneo lake nakudai mkuu wa maji wa wilaya ya Monduli astaafishwe kwa kutokujali wananchi kwakukosa maji kwa miezi yote

"Mkuu wetu wa Wilaya anafanya sana kazi ila wanaomuangusha ni hawa watu wa chini tunaomba wa Wizara watuondolee huyu meneja astaafishwe kwakutokujali wananchi kwasababu nchi yetu haina vita kwanini tukose maji kwa kipindi chote hiki" alisema

Tulizungumza na Diwani wa Kata ya Engutoto Nelson Lowasa, ambaye amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu katika kata yake na kata nyingine za jirani. Anaeleza kuwa jambo hilo wameshalijadili katika baraza la madiwani na kuchakatwa na baraza kuazimia kuwa jambo hilo kutojitokeza tena kwani limekuwa kero kwa wananchi wa Monduli ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri alitoa ufafanuzi ambao mpaka sasa hawajapata majibu.

“Haingii akili kweli mtambo unahudumia wananchi zaidi ya laki mbili kukosa kipuri cha ziada (spare) inaonekana kuna changamoto ama uzembe fulani kwenye mamalaka ya maji AUSWA ila mpaka sasa hatujui nini kinachoendelea” Alisema Lowasa

“Punda zinakatiza katika viunga vya mji wetu wa monduli zikiwa zimebaba maji tunapata wakati mgumu sana maana mashine imeanza kusumbua kitambo zaidi ya miezi mitatu sasa wananchi hawana maji ya bomba watu wa AUSWA wanasema mashine imefeli na wameagiza nyingine ufaransa na walitegemea august 31 ya mwezi ulioisha ingefika ila mpaka sasa wananchi wanataabika na kuendelea kuumia na ile pampu haijafika mpaka sasa” Alisema Diwani Lowasa

Pia tulipata nafasi ya kuzungumza na Mbunge wa Jimbo la Monduli Mh Fredrick Lowassa ambapo alikiri kufahamu na kutambua adha inayowakuta wananchi wakena kwamba tatizo hilo ni la muda mrefu. Mheshimiwa Lowasa alitanabaisha kuwa wamelifanyia kazi na wanaendelea kukamilisha mikataba mikubwa ambayo itapelekea eneo la Monduli kuondokana na changamoto ya maji kubaki kama historia. 

“Changamoto hii imetokea na kufanya maisha ya wananchi kuwa kwenye hali tete kutokana na pampu ya maji kwenye kisima kule Ngaramtoni kuharibika ila serikali inaendelea kufanya juhudiii za kuitengeneza,lakini pia badoo maji hayatoshi tayari pampu zingine zimeshaagizwa kwaajili ya janga hilo kubwa kuondoka kwa wananchi wa Monduli” Alisema Lowasa 

Hata hivyo aliwaomba wananchi wa Monduli kuwa na utulivu kutokana na jambo hilo kwani tayari serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia suluhu Hassan imeanza kulishughulikia kwakuagiza Pampu za maji na tayari zipo njiani na muda wowote kuanzia sasa zitafika na kufungwa na kuendelea na huduma yam aji safi kama hapo awali.

"Mimi nitaendelea kuisihi serikali kulishughulikia na kutatua jambo hili kwa haraka kwasababu ni janga kubwa kwa wapiga kura wangu” Aliongezea

Tatizo la kukosekana kwa maji katika Kata nne za Wilaya ya Monduli ni pampu inayosukuma maji kutoka Mji wa Ngaramtoni kuharibika na kusababisha kukosekana kwa maji kwa kipindi kirefu. Wananchi wamedai walielezwa kuwa mnamo tarehe 02/07/2023 jambo hilo lingekuwa limetatuliwa lakini mpaka sasa halijatatuliwa. Mbaya zaidi watu wa kusoma mita wamekuwa wakipita kwa kipindi hicho chote na kusoma mita na kutuma Ankara ya maji ingawa maji hayatoki chote na kulazimika kulipia shilingi elfu moja.

Bi.Kalista amesema kuwa changamoto hiyo imewaletea shida ya ukame na kuwasabisha wao kununua maji kwa kuletewa kwa maboza ama madumu ambapo kwa kila dumu wanauziwa kwa shilingi elfu moja, kitendo ambacho kwa mkazi mwenye familia na kipato cha chini hawezi kuimili garama hiyo.

Bi Kalista aliongezea kuwa maji yanayosambazwa na serikali yamepita mara moja tu tangu adha hiyo ilipotokea "Gari ya serikali ilikuja mara moja tu kutupa maji na maji yenyewe tunapata ndoo tano tu kwa kila familia, na cha kushangaza wanatuletea lita elfu tano ndio tunagawana kwa kweli tunateseka sana" alisema Kalista

“Nimuombe Rais samia asikie kilio chetu hichi sisi wana Monduli haiwezekani mashine ya kusambaza maji kwenye Wilaya yetu hii iharibike tukose maji kwa zaidi ya miezi mitatu ina maana hawa watu (AUSWA) hawana Kipuri cha akiba mpaka waagize nje ya nchi” Aliongezea

Kwa upande wake Bw.Thomas Laizer Mjumbe wa nyumba kumi  naye aliwaasa viongozi wa juu kujali jamii na kutokuwa wabinafsi kwasababu inawasababisha sisi viongozi ngazi za mitaa na nyumba kumi kuwa na hali ngumu kwa wananchi kwa makosa ya watu wachache wanaofanya uzembe katika nafasi zao za kazi.

“Ni kweli wametoa magari ya kusambaza maji safi kwenye hizi kata zinazohudumiwa na AUSWA lakini magari hayatoshi maana wananchi ni wengi na wana uhitaji wa maji” AliongezeaShare To:

Post A Comment: