Taasisi ya Utafiti  wa  Wanyamapori  Tanzania  (TAWIRI) kwa kushirikiana na  (TANAPA)  imeanza zoezi la kuyaachia makundi manne ya  Mbwa mwitu wapatao ishirini (20) katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa lengo la kuendeleza mfumo ikolojia kwa ustawi wa uhifadhi na kukuza utalii.

Akizungumza wakati wa  zoezi hilo  ambalo limefanyika katika eneo la Makoma Serengeti, Dkt.Emmanuel  Masenga  ambaye ni Mtafiti  Mkuu  TAWIRI  na Mkurugenzi  wa  Kituo  cha  Utafiti  wa Wanyamapori Serengeti  amesema zoezi la kurejesha Mbwa mwitu  katika hifadhi ya Taifa Serengeti  ni endelevu  kutokana na  umuhimu  wa  wanyamapori  hao katika mfumo wa Ikolojia.

Dkt.Masenga  amesema    wataendelea kuwafuatilia mbwa hao  kupitia visukuma mawimbi  baada ya kuwaachia ikiwa ni kuhakisha  azma ya Serikali  ya kuwarejesha kwa wingi mbwa mwitu  ndani  ya  Hifadhi   ya Taifa Serengeti  inatimia kwa ajili ya kutunza bioanuwai hii isitoweke.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda B. Moronda kutoka TANAPA  amesema zoezi hilo kuwarejesha  mbwa mwitu  ndani ya  Hifadhi  ya  Taifa Serengeti  lina manufaa katika uhifadhi kwani  kuongezeka kwa Mbwa mwitu ni zao zuri la utalii, na watalii wataweza kufurahia na kushuhudia namna wanyamapori hawa wanavyowinda tofauti na ilivyozoeleka kuwaona Simba.

Aidha, Maronda  ametoa wito kwa  wananchi wanaopakana na hifadhi  kutoa taarifa pale wanapowaona Mbwa mwitu katika maeneo  yao  na kutokuwaua kutokana na uwepo wa idadi ndogo ndani ya Hifadhi.

Share To:

Post A Comment: