Afisa Elimu Msingi katika Manispaa ya Singida, Omary Maje akifafanua jambo wakati wa mahojiano na Mwandishi wa habari hii yaliyofanyika hivi karibuni mjini hapa.

Na Abby Nkungu, Singida

HALMASHAURI ya  Manispaa ya Singida imetekeleza kwa asilimia 99 agizo la Serikali lililotolewa hivi karibuni kuwataka wamiliki wa mabasi yote ya kubeba wanafunzi wa shule za Awali na Msingi kuwa na mhudumu wa kike na wa kiume wakati wa kuwapeleka shule na kuwarejesha nyumbani.

Lengo la hatua hiyo ikiwa ni kuimarisha suala la ulinzi na usalama wa mtoto kutokana na kuanza kukithiri vitendo vya ukatili wa kijinsia, ikiwemo ubakaji na ulawiti; hasa kwa  watoto walio chini ya miaka minane ambao bado hawana nguvu wala uwezo wa kujitetea kutokana na umri wao mdogo.

Afisa elimu msingi katika Manispaa hiyo, Omary Maje alisema kuwa baada ya kupata agizo hilo la Serikali waliwaandikia barua wamiliki wa shule zote 22 zenye mabasi ya kubeba wanafunzi kuzitaka kutekeleza haraka agizo hilo ambapo hadi sasa ni shule mbili tu ndizo bado kutekeleza.

“Pamoja na kuwa ni agizo la Serikali, kwetu sisi tumelichukulia kama sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) iliyoanza Januari 2021 ambayo inaangalia masuala ya elimu, afya, lishe bora, ulinzi na usalama wa mtoto chini ya miaka minane. Ndio maana ikawa rahisi kuhusisha wadau na kufanikiwa kwani kulikuwa na msingi tayari” alisema Maje.

Aidha alifafanua kuwa, kwa shule ambazo bado hazijatekeleza agizo hilo zimeandikiwa tena  kukumbushwa na kutakiwa kufanya hivyo haraka kabla  ya hatua kali kuchukuliwa dhidi yao.

Meneja wa Mamlaka ya kudhibiti Usafirishaji wa Ardhini (LATRA) mkoa wa Singida, Laila Daffa alisema kuwa wamewatumia barua wahusika wote kuhusiana na agizo hilo na kwamba wataanza kufuatilia utekelezaji wake mara shule zitakapofunguliwa.

“Ni muhimu sana kuwa na Patron na Matron kwenye kila basi la wanafunzi kwani dunia ya sasa imeharibika. Hawa makondakta wanaoitwa na watoto wetu 'anko'  baadhi yao sio waaminifu. Hukawii kusikia mtoto kabakwa au kalawitiwa. Kwa hiyo, tutasimamia utkelezaji wa agizo hilo ipasavyo” alisisitiza.

Hata hivyo, Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani cha Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, Nestory Didi alisema ni muhimu agizo hilo likatungiwa sheria au kanuni ili iwe  rahisi katika utekelezaji wake.

“Kimsingi, sisi kama wasimamizi wa usalama barabarani hatuna nguvu ya kisheria kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa kutokana na ukweli kwamba hakuna sheria wala kanuni yoyote kuhusiana na hilo. Limekaa kama ushauri tu kwa wamiliki wa shule zenye mabasi ya wanafunzi; hivyo ni muhimu kuangaliwa upya kwa sheria au kanuni badala ya agizo pekee ili iwe rahisi kutekelezeka” alisisitiza.

Kwa upande wao, wamiliki wa shule wanasema hilo ni suala la bajeti mpya inayotakiwa kuingizwa kwenye ada inayolipwa na mzazi au mlezi tangu mwanzo wa muhula; hivyo ni vigumu kutekelezeka kwa wakati huu.

“Mimi barua yao nimeiona lakini kwa kweli sijatekeleza na sijaona shule yoyote iliyotekeleza maana ni ghafla mno. Ebu fikiria mimi nina mabasi matano. Kuwepo mhudumu kwa kike na kiume kila basi maana yake unazungumzia ajira mpya ya watu 10. Labda, uwanyonye kwa kuwalipa 100,000/- tu kwa mwezi hapo ni shilingi milioni moja. Je, kwa mwaka mzima ni kiasi gani?" alihoji mmoja wa wamiliki wa shule binafsi ambaye hakutaka kutajwa jina kulinda taasisi yake.

Alisema kuwa ni vyema Serikali ingekaa na wadau wake ambao ni  wamiliki wa shule kuzungumzia suala hilo na umuhimu wake pamoja na changamoto za kibajeti zinazojitokeza badala ya kutoa agizo pekee.

Wakati wamiliki wa shule wakilia na changamoto za kibajeti, baadhi ya wazazi na walezi wanasema agizo hilo limekuja wakati muafaka kwani kuna tishio kubwa la vitendo vya ukatili wa kijinsia; hasa kwa watoto wa kiume ambao wanalawitiwa na wa kike kubakwa ovyo.

“Sio tu wahudumu wa kike na kiume bali agizo liainishe kabisa wawe watu wazima, wenye maadili mema na sifa nyingine  maana watoto wetu wanatoka saa 11:30 alfajiri eti  wanakuwa na 'anko' tu kwenye gari sio sawa......huwa tunakaza moyo tu na kuomba Mungu, Serikali imeona mbali, isimamie utekelezaji kwani sijaona kwenye shule anayosoma mwanangu” alisema Neema John mkazi wa Ginnery Singida mjini.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Bakari Juma mkazi wa Utemini na Issa Rashid wa  Bomani Singida mjini ambao wanasema dunia ya sasa sio ya kuwaacha watoto kwenye gari peke yao na huyo 'anko'.

“Utasema  wapo wengi kwenye basi. Hapana, kuna anayechukuliwa wa kwanza kila siku asubuhi au anayeshushwa wa mwisho maana yake kuna muda wanakuwa wawili tu na anko na anaweza kupanga aanzie wapi na kumalizia wapi. Ni muhimu  kuwa na Patron na Matron mwanzo hadi mwisho wa safari” anasema Baraka na kuungwa mkono na Issa.

Takwimu za Jeshi la Polisi nchini zinaonesha kuwa idadi ya watoto wanaolawitiwa imeongezeka mara mbili zaidi kwa kipindi cha miaka mitano kutoka 537 mwaka 2016 hadi kufikia 1,114 mwaka juzi 2021.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Singida, Nestory Didi ( kushoto) akiwa kazini


 Wanafunzi wakiwa wanaingia kwenye basi tayari kupelekwa shuleni  ( PICHA kwa hisani ya mtandao)

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: