Na. Jacob Kasiri - Mbarali

Kamishna Msaidizi wa Ardhi - Mkoa wa Mbeya, Syabumi Mwaipopo ameiambia Kamati ya  Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuwa serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imerejesha hekta 74,432 kwa wananchi wa Mbarali  ili waendeleze kilimo na ufugaji lengo la kujikwamua kiuchumi tofauti na awali  ambapo maeneo hayo yalikuwa chini ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.

Kamishna Mwaipopo ameyasema hayo leo alipokuwa akiwasilisha ripoti kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea Shamba la Kapunga lililoko wilayani Mbarali kufanya tathmini ya utekelezaji wa uwekaji wa mpaka unaoendelea katika wilaya za Mbarali na Chunya mkoani Mbeya.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) alisema kuwa baada ya kamati hii kutembelea uwandani na kujionea hali halisi itawasilisha mapendekezo ya walichokiona bungeni ili kubadili GN.28 na kuja na GN. mpya ambayo itakuwa ni suluhu kwa mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 18.

"Ndugu zangu wana Mbarali, eneo lote hili lilorudishwa kwenu lilikuwa chini ya uhifadhi,na hivyo serikali kulitoa kwenu ina dhamira ya dhati kwa wananchi wake. Niwaombe, acheni zoezi hili liendee na kukamilika kwa wakati  ili muweze kufanya shughuli zenu za kilimo na ufugaji kwa manufaa yenu na taifa kwa ujumla" alisema waziri.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera akiwakaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii alisema kuwa ni kweli kama wananchi wanavyolalamika shamba la Kapunga halijapunguzwa. Shamba hili halikupitiwa na GN ya zamani na hata hii mpya haijapita pia kwa sababu GN mpya inapita katika maeneo yale yale yaliyopitiwa na GN.28 na wala haianzishi maeneo mapya. Hata, hivyo wananchi watambue kuwa Kapunga Estate ni shamba la serikali na huyu mwekezaji amepewa awekeze tu kwa muda maalum, na mkataba wake utakapoisha shamba hili litarudi serikalini.


Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe.Timotheo Paul Mnzava alisema kamati  hii ya Bunge  inasimamia shughuli za Maliasili na Ardhi kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  hivyo basi msingi wa safari hiyo ni kujiridhisha ili kulishauri Bunge kuona namna bora  kumaliza hili jambo. Aidha, mwenyekiti huyo aliongeza kuwa nchi ni yetu sote lazima tulinde wananchi wetu na pia tulinde Maliasili zetu kwa ajili ya kizazi cha sasa na  kizazi kijacho.

Zoezi la uwekaji mpaka wilaya za Mbarali na Chunya limekamilika, ambapo vigingi 671 vimewekwa kwa umbali wa kilometa 344  kwa uwiano wa mita 500 kila kigingi ili kuwawezesha wananchi na wahifadhi kutambua maeneo yao ili kuepusha muingiliano.Share To:

Post A Comment: