Na. Brigitha Kimario - DODOMA 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa amesema kuongezeka kwa idadi ya watalii kitaifa kumevunja rekodi ya mapato katika Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA). 

Ameyasema hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika Bunge la 12, mkutano wa 11 kikao cha 39 jijini Dodoma. 

“ Taasisi  za utalii nchini zimevunja rekodi ya mapato katika maeneo yao mfano TANAPA kwa mwaka mzima wa 2021/22 walikusanya TZS bilioni 174, kwa miezi 10 tu ya mwaka huu wa fedha, wameshakusanya TZS Bilioni 291 mapato haya kwa taasisi ni makubwa kuliko yoyote yaliyowahi kukusanywa tangu zianzishwe.”

Aidha, mapato haya yametokana na juhudi zilizofanyika za pamoja kutangaza vivutio vya utalii na kuimarika kwa miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi.

Aliongeza kuwa Shirika litaendelea na juhudi zote kuimarisha shughuli zake za ulinzi, ikolojia, kutangaza utalii, kukusanya maduhuli na kuimarisha miundombinu ili tuendelee kuvunja rekodi na watalii kufurika zaidi katika hifadhi zetu.

“ Shirika litaendelea kuboresha miundombinu ya huduma za utalii kwa kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 500 na kukarabati kilometa 10,500. Vilevile shirika litakarabati kilomita 300 za njia ya miguu za kupanda milimani; kujenga mifumo ya usambazaji wa maji safi na malango 10 ya kukusanya mapato katika hifadhi za Taifa Ibanda-Kyerwa (1), Serengeti (2), Kilimanjaro (1), Tarangire (1), Ruaha (1), Katavi (1), Nyerere (1), na Mikumi (2). 

Pia, Shirika litajenga studio ya kurusha vivutio vya utalii mubashara utakaowezesha vivutio kurushwa moja kwa moja kwenye mitandao na chaneli za kimataifa.”

Wizara ya Maliasili na Utalii leo imewasilisha makadirio ya Bajeti ya jumla ya Shilingi 654,668,208,000 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 matumizi ya fungu 69 kwa mwaka wa fedha. Kati ya fedha hizo TZS 486,501,449,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na TZS 168,166,759,000 ni za miradi ya maendeleo.
Share To:

Post A Comment: