NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya), Dkt. Wilson Charles Mahera amewaelekeza waganga wakuu wa mikoa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri kusimamia kikamilifu utaratibu wa mfumo wa ugavi kwenye bidhaa za afya.

Dkt. Mahera ameyasema hayo leo tarehe 03 Mei 2023 kwenye kikao kazi kilichowakutanisha Waganga Wakuu wa Mikoa na Wafamasia kilichofanyika jijini Dodoma.

Kikao hicho kimelenga kufanya tathimini ya ufuatiliaji na maendeleo katika utekelezaji na maboresho ya matumizi ya takwimu katika mikoa kupitia mbinu ya “Impact approach”.

“Sisi viongozi tuna jukumu la kusimamia timu za mikoa, halmashauri na za vituo vya kutolea huduma za afya ili viweze kuboresha upatikanaji wa bidhaa kupitia takwimu sahihi, maoteo ya bidhaa yaliyo sahihi na matumizi ya fedha kwa kuzingatia miongozo.”

Dkt. Mahera pia amewataka kuhakikisha wanatumia takwimu katika kufanya maamuzi hatua ambayo itasaidia kupunguza changamoto zinazotokana na usimamizi hafifu wa bidhaa hizo.

Pia amewataka kufanya ufuatiliaji wa utoaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, Dkt. Mahera amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI inaendelea na mikakati kabambe ya kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa asilimia 100.

“Tunamikakati ya kuhakikisha dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara unakua wa uhakika na kwa asilimia 100 ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wananchi.”

Dkt. Mahera pia amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kutumia takwimu.

“Hatua hii itasaidia kudhibiti upotevu na matumizi mabaya na kuimarisha matumizi sahihi ya nyenzo za mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya.”

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi katika kumarisha utoai wa huduma za afya ngazi ya msingi.”

Dkt. Mahera ametumia fursa hiyo kukemea tabia ya wizi wa vifaa tiba ambao unafanyika katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya na kutolea mfano matukio ya wizi katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda na Kituo cha Afya Ilembula wilayani Wanging’ombe na kusisitiza kuwa tayari watu kadhaa wanashiliwa ili kuchukuliwa hatua.

Share To:

Post A Comment: