Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa taasisi za fedha nchini hususani Mabenki kuwafikia vijana wanaopata ujuzi katika vyuo mbalimbali vya ufundi stadi hapa nchini ili kutoa mikopo na kuwawezesha vijana hao kupata vifaa vitakavyosaidia kuendeleza shughuli wanazozifanya.

 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia Viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro kwenye hafla ya Ufunguzi wa Chuo cha Veta cha Wilaya ya Ngorongoro kilichopo Kijiji cha Samunge leo tarehe 17 Mei 2023. Amesema serikali inalenga kujenga vyuo vya Veta kila Wilaya hivyo ni vema taasisi za kifedha kuona umuhimu wa kuwawezesha mikopo nafuu itakayowasaidia vijana kufanya biashara kirahisi.

 

Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Samunge kwa utaratibu wao wa kujitolea katika maendeleo hususani kwa kuanzisha mradi huo wa Chuo cha Vet ana miradi mingine.  Amesema chuo hicho ni mkombozi kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na lengo la serikali ni kuhakikisha wale wote wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari wanapata ujuzi utakaoweza kuendeleza maisha yao na kutoa mchango kwa taifa.

 

Ameongeza kwamba serikali inatekeleza kwa vitendo ilani ya chama cha mapinduzi inayosisitiza umuhimu wa elimu kwa kuhakikisha unafanyika uwekezaji katika akili ya mwanadamu na kukuza ujuzi ili kujiletea maendeleo ya haraka na kutumia vema rasilimali zilizopo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa eneo la Wasso Wilayani Ngorongoro waliojitokeza kwa wingi katika eneo la Uwanja wa Ndege kwa lengo la kumuaga akimaliza ziara yake wilayani humo.

 

Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa eneo hilo kuwa na subira wakati serikali ikifuatilia kwa karibu suala la madai ya mifugo kukamatwa nje ya hifadhi kwa kuwa serikali itafungua majadiliano na wananchi wa eneo hilo ili kuondoa sintofahamu hiyo.

Amesema kwa mujibu wa sheria mifugo yote itakayoingizwa ndani ya hifadhi lazima itakamatwa na hatua kuchukuliwa na kinyume na hapo mifugo haipaswi kukamwatwa nje ya hifadhi. Aidha amewataka wananchi wa Ngorongoro kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi hali inayopelekea kudhurika kwa baadhi ya askari wa hifadhi wanapotekeleza sheria. Pia amewaagiza kutunza amani iliopo kwa kuishi kwa misingi ya sheria na taratibu za nchi.










Share To:

Post A Comment: