Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WAKAGUZI walioteuliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na weledi katika kudhibiti ubora na ufanisi wa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA ili kulinda afya za wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga alipokuwa akifungua kikao kazi cha wakaguzi wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo Tanzania jijini Dodoma.

Dkt. Mganga alisema “napenda mfahamu kuwa utendaji kazi wowote hupimwa kwa taarifa. Hivyo, mwongozo wa kukasimu madaraka na majukumu umebainishwa wazi kuwa taarifa za utendaji kazi za robo mwaka na taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya utendaji kazi za udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA katika soko zinatakiwa kuandaliwa na kutumwa TMDA kupitia viongozi wenu katika ngazi ya halmashauri. Nimatumaini yangu mtafanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa”.

Katibu Tawala huyo aliwataka washiriki wa mafunzo kutumia mafunzo hayo kuboresha utendaji kazi wao. “Kupitia mafunzo haya mkatatue changamoto zinazojitokeza mara kwa mara na hivyo, kusaidia wakaguzi wa halmashauri kutotumia nguvu nyingi nyakati za kaguzi ambazo husababishwa na kutokutoa elimu kwa wateja. Hivyo, kukinzana na utaratibu wa ukaguzi wa TMDA ambao umejikita zaidi katika kuelimisha na kuwezesha” alisema Dkt. Mganga.

Nae Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya kati, Sonia Mkumbwa aliwakumbusha wakaguzi hao kutumia sheria, kanuni na miongozo katika utoaji huduma. “Nitoe rai kwa wataalam wote kwenye kada ya Afya kuendelea kufuata sheria, kanuni na miongozo katika utoaji wa huduma. Kwa kuhakikisha bidhaa ambazo wanazitoa wao wenyewe kabla ya kumpa mtu uhakikishe kwamba umeiangalia na inakidhi matakwa ya ubora na usalama ndiyo umpe mtumiaji. Lakini pale utakapopata changamoto yoyote sisi TMDA tupo kwenye kanda nane na taifa kwa ajili ya kutoa msaada. Mfamasia, mtaalam wa maabara na daktari kwenye halmashauri husika ni muwakilishi wa TMDA kama sisi tupo mbali” alisema Mkumbwa.

Akiongelea mafunzo hayo, aliyataja kuwa yanalenga kwenda kutatua changamoto katika maeneo ya kutolea huduma. “Sehemu za kutolea huduma kuna bidhaa zenye ubora tofauti. Mfano bidhaa bandia na bidhaa duni. Kuna bidhaa nyingine tarehe ya kutumika bado ipo vizuri lakini kutokana na uhifadhi wake kuwa duni hakuna feni au kiyoyozi jambo linalosababisha kiwango cha ubora katika bidhaa ile kushuka” alisema Mkumbwa.

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba kanda ya kati inahudumia jumla ya halmashauri 29 ikiwa ilianzishwa mwaka 2012.

Share To:

Post A Comment: