Virusi vya Marburg ni ugonjwa hatari wa mlipuko unaosababishwa na virusi vya Marburg ambavyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa na  saba kati yao kufariki mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt Ujerumani na Belgrade huko Serbia.

Miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo yamewahi kukumbwa na ugonjwa huu ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Afrika Kusini, Uganda, Zimbabwe na Angola.



Dalili

Dalili za awali ni pamoja na homa, kuumwa vibaya na kichwa na Kuumwa na misuli, dalili za baadaye ni kikohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu katika mwili.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema Baadhi ya watu hutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili na kufa siku nane hadi tisa baada ya kuugua kwa sababu ya kupoteza damu nyingi na mshtuko.

Kwa wastani, virusi huua nusu ya walioambukizwa, WHO inasema, lakini aina hatari zaidi imeua hadi 88%.



Unavyoenea

• Popo, nyani na nguruwe wanatajwa kueneza ugonjwa huu.

• Kwa wanadamu ugonjwa huu huenea kupitia maji ya mwili.

• Hata watu wakipona, damu zao, zinaweza kuwaambukiza wengine kwa miezi mingi baadaye.


Matibabu

Hakuna chanjo maalumu wala matibabu ya virusi hivi.


Namna ya kujikinga

• Epuka kula au kushika nyama ya porini katika maeneo yenye mlipuko.

• Epuka kuwa karibu na nguruwe katika maeneo yenye mlipuko, WHO inasema.

• Wanaume ambao wamekuwa na virusi wanapaswa kutumia kondomu kwa mwaka mmoja baada ya kupata dalili au hadi mbegu zao zitakapothibitishwa mara mbili kuwa hazina virusi.

• Kwa wale wanaozika watu ambao wamekufa kutokana na virusi wanapaswa kuepuka kugusa mwili.



 Milipuko mikubwa kuwahi

2017, Uganda: visa - 3, Vifo - 3

2012, Uganda: visa - 15, Vifo - 4

2005, Angola: visa 374, Vifo - 329

1998-2000, DR Congo: visa - 154, Vifo - 128

1967, Ujerumani: visa 29, Vifo - 7. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN).

Share To:

Post A Comment: