Wakazi wapatao 4251 katika Vijiji vya Kibogoji na Pandambili Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wataondokana  na adha ya maji iliyowakabili kwa muda mrefu baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa maji wenye thamani zaidi ya shilingi milioni 530.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa akizungumza na wakazi hao mara baada ya uzinduzi wa mradi huo, amewataka kila mmoja kuchukua jukumu la kulinda vyanzo cha maji na miundombinu ya miradi ya maji inayotekelezwa na serikali kwenye maeneo yao.

Mwassa amesisitiza kuwa serikali inatumia gharama kubwa kutekeleza miradi hiyo, hivyo mwananchi anao wajibu wa kutoa taarifa za hujuma yoyote pale zinapojitokeza.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Sospeter Lutonja, amesema bado wanakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya maji kwa kiasi kikubwa, shughuli za kibinadamu hasa kilimo na mifugo zikiwa tishio.

Amesema kwa mwaka huu wa fedha RUWASA inaendelea kutekeleza miradi hamsini ya maji katika vijiji 127 mkoani humo ambapo wananchi zaidi ya laki mbili watanaufaika na miradi hiyo ifikapo mwezi Juni, 2023.

Mradi wa maji Kibogoji ni mradi ambao  umeibuliwa kutokana na mahitaji ya wakazi waishio Kata ya Kibati Wilayani Mvomero, kukamilika kwa mradi huu kutawaondolea adha ya kutumia muda mwingi  wananchi kuteka maji katika mabwawa na visima vya kunyweshea mifugo vinavyozunguka maeneo hayo.

Share To:

Post A Comment: