Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.


Sehemu ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Manispaa hiyo.


Sehemu ya Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Manispaa hiyo.


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe. Jaffrery Naigesha akitoa shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya Naibu Waziri huyo kumaliza kuzungumza na watumishi wa Manispaa hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Bw. Elihuruma Mabelya akitoa shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya Naibu Waziri huyo kumaliza kuzungumza na watumishi wa Manispaa hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.

*********************

Na. Veronica E. Mwafisi-Temeke na Ubungo

Tarehe 18 Disemba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watumishi wa umma kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika maeneo yao ya kazi bila kusimamiwa na viongozi wa ngazi za juu kwani ni wajibu wao kuhakikisha miradi inayotekelezwa na Serikali inakamilika kwa wakati kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekusudia.

Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Ubungo, Mhe. Ndejembi amesema, kuna baadhi ya maeneo usimamizi wa miradi ya serikali ni hafifu hivyo inamlazimu Mkuu wa Wilaya au Mkurugenzi wa halmashauri aende kuhimiza usimamizi wa miradi.

“Hakuna mradi wa umma au wa Serikali ambao hausimamiwi na mtumishi wa umma, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi wa umma katika eneo lake na kwa nafasi yake kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na Serikali kwa manufaa ya taifa,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, miradi yote inayotekelezwa na Serikali ina umuhimu kwa wananchi katika eneo la utoaji wa huduma za afya, elimu na nyinginezo, hivyo ni lazima watumishi wa umma waisimamie kikamilifu.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe. Jaffery Naigesha amemshukuru Mhe. Naibu Waziri Ndejembi kwa maelekezo mbalimbali ya kiutumishi aliyoyatoa, na kuongeza kuwa anaamini yatawajenga kiutendaji watumishi wa umma.

Mhe. Naigesha amemweleza Mhe. Naibu Waziri Ndejembi kuwa, mafanikio yote ambayo Manispaa ya Ubungo imeyapata yanatokana na fedha za utekelezaji wa miradi walizopatiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Bw. Elihuruma Mabelya amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi walio katika wilaya yake.

Bw. Mabelya ameahidi kuwaongoza watumishi wa halmashauri yake katika kusimamia miradi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: