Muonekano wa vifaa vilivyopokelewa na Bohari ya Dawa (MSD) 

Na Mwandishi Wetu 

Katika kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani MSD imeendelea kupokea na  kusambaza bidhaa mbalimbali za afya za kupambana na kudhibiti maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai ameeleza kuwa miongoni mwa bidhaa za afya ambazo kwa sasa inauhitaji mkubwa na inaendelea kusambazwa na MSD kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ni vipimo vya kupima maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na gonjwa la zinaa la Kaswende ( HIV/ Syphilis Duo).

Vipimo hivyo vinafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa  kupambana UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria  (The Global Fund) na pia hutumika kupima akina mama wajawazito kutambua maambukizi ya magonjwa yote mawili kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa Dr. Ibadi Kaondo wa MSD, vipimo hivyo vinamsaidia mama mjamzito kutambua hali ya afya mapema, na endapo maambukizi yamegundulika inarahisisha  kuanza matibabu  mapema ili kufubaza makali ya virusi vya ukimwi na kutibu kaswende kwa ajili kuimarisha afya ya mzazi na kumkinga mtoto dhidi ya Maambukizi ya VVU, Kaswende ama kujifungua mtoto mfu.

Hapo awali vipimo hivi kila kimoja kilikuwa kinajitegemea, ambapo vilitumia muda mrefu kutoa  majibu.  MSD kwa sasa ina shehena ya kutosha ya vipimo hivyo ambavyo tayari  baadhi vilishaanza kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Moja ya kifaa kilichopokelewa.
Vifaa hivyo vikiwa kwenye maboksi


Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: