Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) pamoja na wajumbe wa kamati ya Kitaifa ya wataalamu inayosimamia uboreshaji wa Mitaala ya Elimumsingi, Sekondari ya Juu na Ualimu leo tarehe 29/11/2022 imetembelea Bodi ya Elimu ya Nchini Rwanda (Rwanda Basic Education Board) kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa  Mitaala yenye kujenga ujuzi.


TET ipo katika ziara nchini Rwanda kuanzia tarehe 28/11/2022 hadi 2/12/2022  kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu maboresho ya Mitaala yanayoendelea nchini.


Katika ziara hiyo Bi Joan Murungi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Elimu Rwanda (REB) aliwasilisha kazi mbalimbali zinazofanywa na Bodi hiyo na namna Rwanda inavyotekeleza mitaala inayojenga umahiri  ( Competence Curriculum Based)


Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Kitaifa ya Mitaala Prof.Makenya Maboko amesema kuwa,Serikali ya Tanzania kupitia TET kwa sasa ipo inafanya maboresho ya mitaala itakayosaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira  kwa kumuandaa mhitimu mwenye ujuzi wa kujiajiri na kumudu maisha ya siku kwa siku.


"Tumekuja kujifunza nchini namna Rwanda inavyoandaa na kutekeleza Mitaala yenye kumjengea mwanafunzi ujuzi. Hili ndilo lengo la kufanya mapitio haya makubwa ya mitaala na kiu ya wadau wengi ni kuwa na mitaala itakayowawezesha wahitimu kuwa na ujuzi". Amesema Prof.Maboko.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt.Aneth Komba amesema, uzoefu utakaopatikana utasaidia katika mapitio ya mitaala yanayoendelea.


"Kwa sasa tayari TET tumeandika rasimu ya mtaala na mihutasari lakini tumekuja hapa kupata uzoefu juu ya uandaaji na utekelezaji wa mitaala yenye kumjengea mhitimu uwezo wa kujiajiri na kumudu maisha ya kila siku" Amesema Dkt.Aneth.


Nchi ya Rwanda imefanya maboresho ya mtaala mwaka 2015 na kuweza kuwa na Mitaala inayozingatia ujenzi wa umahiri.

Share To:

Post A Comment: