Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza na Wakaguzi wa ndani 140 kutoka halmashauri 69 nchini( hawapo pichani), wanaoshiriki mafunzo ya siku tatu ya namna ya kukagua kwa ufanisi taarifa za fedha, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali katika Kituo cha Mikutano cha NBAA, Bunju, Dar es Salaam.


 Na Josephine Majula na Scola Malinga WFM – DSM


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewataka Wakaguzi wa Ndani kufanya kazi zao bila kupepesa macho kwa kufichua upotevu wote wa fedha za umma kwa kuwa Serikali ipo na itawalinda ili kuhakikisha fedha za umma vinatumiwa vizuri kama ilivyopangwa

Dkt. Nchemba ametoa maelekezo hayo wakati akifungua mafunzo ya Siku tatu ya Wakaguzi wa Ndani wapatao 140 kutoka Halmashauri 69 nchini, kuhusu ukaguzi wa taarifa za fedha kutoka katika Taasisi za Umma yanayofanyika katika Kituo cha NBAA, Bunju, Jijini Dar es Salaam.

“Wekeni wazi upotevu wote wa fedha za umma katika miradi inayotekelezwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale wote watakaokuwa wametumia vibaya fedha ya umma”, alisisitiza Dkt. Nchemba

Aidha, Dkt. Nchemba aliahidi kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ufinyu wa bajeti, vitendea kazi na wataalamu mbalimbali wakiwemo wahandasi watakaoshiriki katika ukaguzi wa mali za umma Pamoja na kukamilisha muundo mpya wa tasnia ya ukaguzi wa ndani ili kuleta tija.

“Serikali itazifanyia kazi haraka changamoto hizo ili zisiwe kikwazo katika kutekeleza majukumu yenu ya msingi”, alisisitiza Dkt. Nchemba.

Alisisitiza umuhimu wa wataalam hao kuyatumia mafunzo watakayoyapata kuboresha mifumo ya ukaguzi wa ndani kwa sababu kada hiyo ni muhimu kuchangia udhibiti wa matumizi ya serikali kuoitia ukaguzi wanaoufanya.

Kwa Upande wa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Bw. Athumani Mbuttuka, alitoa wito kwa maafisa masuuli kutenga fedha kwa ajili ya ukaguzi katika miradi yote inayoibuliwa ili kupata thamani halisi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

“Kada ya Wakaguzi wa ndani inakabiliwa na changamoto za kibajeti hivyo ninakuomba mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mioango, kuwaelekeza maafisa Masuuli, wakati wanaanda miradi, waweke fungu la ukaguzi katika miradi hiyo, hatua hii itasaidia kupunguza ama kuondoa kabisa malalamiko ya wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi yao” alisema Bw. Mbuttuka

Aidha, Bw. Mbuttuka alielezea umuhimu wa wakaguzi wa ndani kujengewa uwezo na ujuzi wa kufanya ukaguzi kwenye mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo inatumika kwa kiasi kikubwa ili kudhibiti upotevu wa fedha za umma na kuongeza mapato ya Serikali.

“Tumeanza kutoa mafunzo kwa wakaguzi wetu wa ndani ili kuwajengea uwezo wa kufanya ukaguzi kupitia mifumo ambapo hadi kufikia mwaka 2026, tunatarajia kuwa na wataalam zaidi ya 320 watakaopatiwa mafunzo hayo ili kukabiliana na ushindani na mataifa mengine Jirani waliowekeza kwa kiwango kikubwa katika taaluma hiyo” Alisema Bw. Mbuttuka

Kwa upande wao, Mkaguzi Msaidizi wa Ndani Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Subi na mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Kaimu Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, CPA Wamilika Mlangi, waliishukuru Serikali kwa kuendesha mafunzo hayo yatakayo waongezea ujuzi wa kufanya kaguzi mbalimbali kwa ufanisi Zaidi na hivyo kuleta tija katika matumizi ya fedha za Serikali.

Washiriki wa mafunzo hayo wamekubaliana kwenda na kauli mbiu isemayo: Tutakwenda, Tutakagua na Tutatoa taarifa kama ilivyo, baada ya kupewa changamoto hiyo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba

Wakaguzi wa Ndani wapatao 520 kutoka nchi nzima wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo ya ukaguzi wa taarifa za fedha ili kujiridhisha kuhusu usahihi wake kabla ya kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Share To:

Post A Comment: