Na,Mwandishi Wetu,Arusha


Wadau wa shirika la KUKUA PAMOJA TANZANIA, wametoa mashine ya cherehani yenye thamani ya shilingi laki 3 kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Ilkiurei halmashauri ya Arusha kwa ajili ya kushona taulo za kike kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hiyo,Mkurugenzi wa shirika la  TUKUE PAMOJA Tanzania  Ayubu Patrick, amesema kuwa shirika limefikia hatua hiyo ili kuwasaidia wasichana wasio na uwezo wa kupata taulo hizo wakati wa hedhi na kushindwa kuhudhuria masamo yao.

Aidha Shirika kupitia mradi wa Tukue Pamoja, litawafundisha wasichana 20 kushona taulo hizo ili baadaye waweze kushona wenyewe huku taulo hizo zikigawiwa kwa wasichana wote shuleni ambao tayari wamefikia umri wa balehe.

"Tutakuwa na program ya kuwafundisha wasichana 20 kushona wakishaweza, watafundisha wenzao, lakini zaidi tutawafundisha makuzi na mabadiliko ya kukua kimwili na athari zake pamoja na kujitunza katika hali za mabadiliko ya makuzi na ujana". Amesema Mkurugenzi Patrick.


Vilevile ameeleza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa bado wasichana wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kuhudhuria masomo kwa kukosa vipindi 3  hadi 4 kwa mwezi na takribani vipindi 48 kwa mwaka wakati wa hedhi kwa kushindwa kumudu gharama za taulo za kike.

Hata hivyo wasichana hao wamelishukuru shirika hilo kwa msaada huo ambao wamethibitisha ni muhimu kwao kwa kuwa wasichana wengi hushindwa kujiamini kipindi cha hedhi kutokana na kukosa uhakika wa kujisitiri.

Jemima James mwanafunzi wa darasa la 4 amebainisha kuwa ni kweli kuna tatizo la baadhi ya wasichana kushindwa kumudu kununua taulo za kike na baadhi kukosa masomo kipindi hicho cha hedhi na kusababisha kuzorotesha maendeleo ya wasicha kimasomo.

"Kuna wasichana wakiwa kwenye hedhi inawalazimu kuomba ruhusa na kubaki nyumbani tukifundishwa kutengeneza taulo hizo kutaturahisishia hedhi salama pamoja na kusoma kwa amani". Amesema Jemima


Naye Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ilkiurei Mwl.Beatrice Kapinga amesema kuwa wanafunzi wakiwa na uhakika wa kupata taulo hizo shuleni itaongeza hari ya wasichana kusoma kwa kuwa changamoto hiyo haitakuwepo tena.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: