Na Karama Kenyunko 


MRAKIBU Msaidizi wa polisi,(ASP) Lydia Ngau anayeishi Ukonga Mzambarauni na wenzake watatu wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la wizi kwa kutumia jina la Mambosasa

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo leo Septemba 30, 2022 na wakili wa serikali Mwandamizi Sylivia Mitanto imewataja washtakiwa wengine Kuwa ni, mjasiliamali, Mpelembe Mpelembe (41) mkazi wa Mbagala Kijichi, Shabani Hamis (47) Mfanyabiashara anayeishi Ilala Boma na Henry Chambo (30) Driver wa Kiwalani Kijiwesamli.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Yusto Rubologa imedaiwa, Januari 4,2021 huko Tabata Kinyerezi ndani ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliiba sh. 2,560,000 mali ya Abdallah Said Abdallah.

Imeendelea kudaiwa kuwa washtakiwa waliiba pesa hizo baada ya kudanganya kuwa wao ni maafisi wa polisi na wametumwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam Lazaro Mambosasa kwenda kumkamata kujihusisha na utengenezaji wa vyeti feki vya kuzaliwa pamoja na vyeti vya shule huku wakijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo washtakiwa wamekana kutenda kosa hilo.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Octoba 12 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Mshtakiwa ASP Lydia yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini bondi ya shilingi laki tano.


Share To:

Post A Comment: