Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) asisitiza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza wigo na upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo nchini. Mhe. Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 21 Septemba, 2022 katika ukumbi wa St. Gasper Jijini Dodoma alipokuwa akizindua Mradi wa Kuimarisha Huduma za Afya ya Mimea na Usalama wa Chakula nchini unaotekekelezwa na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU).


Mradi huu umekuja wakati sahihi kwani Serikali kupitia Wizara ya kilimo imejiwekea kipaumbele cha kukuza mauzo ya mazao nje kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.2 za sasa hadi Dola Bilioni 5 ifikapo 2030 ( agenda 10/30), alisisitiza Mhe Mavunde.


Sanjari na hilo, Mavunde alieleza kuwa utekelezaji wa Mradi huu pia unaakisi na kuongeza shime katika kufikia vipaumbele vya nchi katika sekta ya kilimo hususan kuhakikisha ukuaji wa sekta ya kilimo unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, hatua ambayo utafikiwa kwa utekelezaji wa mikakati mbalimbali moja ikiwa ni mradi huu.


"Naipongeza sana Mamlaka yetu ya TPHPA kwa kupata Ithibati ya Kimataifa, ambapo sasa ikitoa cheti kwenye bidhaa yeyote kinatambulika dunia nzima, hii ni hatua kubwa sana. Ni matumaini ya Serikali kuwa Mradi huu unaenda kuchagiza maendeleo zaidi na kurahisisha biashara ya mazao nje ya nchi", aliongeza Mhe. Mavunde.


Vilevile, Mhe. Mavunde alibainisha kuwa kukua kwa biashara za kimataifa huenda sambamba na kuongezeka kwa wingi wa watu kuvuka mipaka ya kimataifa na hivyo kuongeza hatari ya kuingia kwa visumbufu hatari na vamizi nchini. Hivyo, kuimarika kwa udhibiti wa afya ya mimea chini ya TPHPA ni muhimu kwa lengo la kuzuia uvamizi wowote unaohatarisha usalama wa chakula na biashara ya mazao nje ya nchi.


Naye Kaimu Mkurugenzi wa TPHPA, Dkr. Efrem Njau alieleza kuwa, Mradi huo wenye thamani ya EURO Milioni 10.1 utatekelezwa kwa Miaka mitatu na nusu, na unataraji kuleta tija mbalimbali ikiwemo kuimarisha mfumo maalum wa udhibiti wa bidhaa zinazoingia na kutoka nje, kuwajengea uwezo wataalam wa afya ya mimea, kujenga, kukarabati na kuweka vifaa kwenye maabara za TPHPA na kuimarisha mfumo wa kufanya savei mashambani na kuweka mfumo wa kidijitali wa kukusanya takwimu za visumbufu vya mimea.

Share To:

Post A Comment: