BALOZI wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema takribani wawakilishi wa Kampuni 1,000 za nchini Italia wamethibitisha kushiriki kwenye Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji linalotarajiwa kufunguliwa rasmi jijini Zanzibar tarehe 28 Septemba 2022.


Akizungumza leo tarehe 27 Septemba 2022 jijini Zanzibar wakati wa mkutano wa maandalizi uliokuwakutanisha Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Italia na Maafisa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoka Sekta zinazosimamia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Kombo amesema mwitikio huo mkubwa wa washiriki wa kongamano kutoka Italia unatokana na jitihada zinazofanywa na ubalozi katika kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na utalii nchini humo.

“Ubalozi wa Tanzania nchini Italia umeendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji, utalii na biashara zilizopo nchini. Ni kutokana na jitihada hizo Kampuni nyingi zimehamasika na kuonesha nia ya kuja kujionea fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zitakazowasilishwa wakati wa Kongamano hili. Nimefarijika sana kuona mwitikio huu wa washiriki kutoka Italia ambao umezidi ule wa kongamano la kwanza” amesema Balozi Kombo.

Kadhalika ameongeza kusema kuwa tayari zipo Kampuni kadhaa za Italia zimewekeza nchini ikiwemo ile ya Toscana Macchine Calzature (TMC) iliyopo mkoani Kilimanjaro inayojishughulisha na uuzaji wa mashine za kisasa na vipuri vyake vya utengenezaji wa viatu na bidhaa na ngozi. Amesema Kampuni hiyo ambayo huzalisha viatu zaidi ya jozi 4,000 kwa siku, imeonesha utayari wa kutoa wataalam saba (7) watakao toa mafunzo ya utengenezaji bidhaa za ngozi katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar.

Vilevile, Balozi Kombo ameeleza kuwa, kutokana na jitihada zinazofanywa na ubalozi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii hapa nchini safari za ndege za watalii kutoka Italia zimeongezeka kutoka safari tatu hadi nane kwa wiki.

Balozi Kombo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa za soko la bidhaa kama Parachichi ambazo tayari zimeanza kuuzwa nchini Italia.

Kwa upande wake, Balozi wa Italia hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji na kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana Tanzania katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.

Kongamano hilo ambalo litafunguliwa rasmi tarehe 28 Septemba 2022, linalenga pamoja na mambo mengine kujadili kwa kina namna ya kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia sekta ya biashara na uwekezaji. Pia kutoa nafasi kwa Tanzania kuainisha fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini zinazoweza kuchangamkiwa na washiriki kutoka Italia.

Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo wa Kongamano la Kwanza la aina hii lililofanyika jijini Rome, Italia mwezi Desemba 2021, linatarajiwa kuhitimishwa jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2022.

Share To:

Post A Comment: