Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Kamati ya kushughulikia migogoro ya ardhi iliyoundwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi itaendelea kutatua changamoto za ardhi katika mkoa wa Dodoma kuanzia siku ya jumatatu tarehe 26 hadi 30 Sept 2022.



Awali kamati hiyo ilisikiliza na kutatua changamoto za ardhi katika mkoa wa Dar es Salaam ambapo zaidi ya changamoto 150 za migogoro ya ardhi zilipatiwa ufumbuzi.



Maeneo ambayo kamati hiyo itasikiliza na kutatua changamoto za migogoro ya ardhi katika mkoa wa Dodoma ni Mkonze, Kikuyu Kaskazini na Kusini, Ipagala na Makole, Makulu na Iyumbu pamoja na maeneo ya Nzuguni, Mtumba na Kikombo.



Akizungumza na waandishi wa habari Sept 23, 2022 jijini Dodoma, katibu Mkuu wa wizara ya Ardhi Dkt Allan Kijazi alisema, lengo la kuanzisha utaratibu huo wa kutatua changamoto za ardhi ni kupunguza migogoro ya ardhi inayolalamikiwa.



Hata hivyo, alisema kuwa, kamati hiyo itakayohusisha taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama haitashughulika na migogoro ya ardhi ambayo kesi zake ziko mahakamani.



Kwa mujibu wa Dkt Kijazi, uzoefu unaonesha migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na uelewa mdogo wa sheria pamoja na taratibu mbalimbali za umiliki jambo alilolieleza kuwa linasababisha wajanja wachache kutumia udhaifu huo kuwalaghai au kudhulukmu wananchi.



“Sababu nyingine ya migogoro ya ardhi ni uuzaji maeneo bila kufuata taratibu pamoja na makosa ya kiutendaji yanayosababishwa watumishi wetu wa serikali wasio waminifu”. Alisema Dkt Kijazi.



Hata hivyo, Dkt Kijazi alitoa rai kwa wananchi kufuata taratibu za kisheria pale wanapotaka kununua ardhi sambamba na wamiliki kufanya maendelezo ya maeneo waliyomilikishwa ndani ya miaka mitatu na kusisitiza kuwa wizara yake hivi karibuni itaanza operesheni maalum ya kubaini wamiliki wasioendeleza maeneo yao.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: