Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ester Chaula (kulia) akitoa taarifa ya ujenzi wa ofisi hiyo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Singida, ambalo ujenzi wake unategemea kukamilika ifikapo Novemba, 2022, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhajj Juma Killimbah akizungumza. |
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akizungumza wakati wa mkutano wa majumuisho wa ziara hiyoya Waziri Mkuu.
Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida Mandewa. |
Na Dotto Mwaibale, Singida
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemaliza ziara yakeya kikazi ya siku mbili
mkoani Singida ambapo ametoa maagizo mazito kwa Wakuu wa Wilaya ya kuhakikisha
wanasimamia watumishi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Singida ambao walikusanya
fedha za mapato lakini hawakuzipeleka benki kuzirudisha haraka.
Majaliwa alitoa agizo hilo jana katika kikao cha majumuisho ya ziara yake hiyo wakati akizungumza na watumishi wa
Halmashauri za Wilaya ya Singida, Ikungi na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Alisema kumekuwa na tatizo kubwa kwenye halmashauri nyingi nchini katika
ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo baadhi ya watumishi wanapokusanya fedha
haziingizi kwenye mfumo wa serikali
jambo ambalo imekuwa kero kubwa.
"Wakuu wa Wilaya hakikisheni watumishi wanaodaiwa fedha wazirudishe
haraka, Iramba, Manyoni na hata Ilongero (Halmashauri ya Wilaya ya Singida)
nimepewa orodha ya watumishi ambao wanadaiwa fedha za makusanyo," alisema.
Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza suala la
ukusanyaji wa mapato na hata majuzi wakati anawaapisha wakuu wa mikoa lakini
cha kushangaza baadhi ya watumishi wa umma wamegeuka kuwa wabadhirifu.
Alisema ujanja unaofanywa na baadhi ya watumishi kufuja fedha za makusanyo
ni kwamba wanapokusanya fedha hasa wanapobaini ni nyingi wanazima mashine ili
zisiingie kwenye mfumo wa serikali.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi kuacha urasimu katika utendaji wa
kazi kwani mambo hayo ndio yanakaribisha vitendo vya rushwa chini.
Kuhusu idara za manunuzi, alisema limekuwa ni tatizo kubwa ambapo idara
hizo zimekuwa zikiweka makadirio makubwa ya bei za manunuzi ya vifaa vya ujenzi
kwenye miradi hususani inayotumia 'force account'.
Aliongeza kuwa kwenye halmashauri kumekuwa na tatizo kubwa la usimamizi wa
miradi inayotekelezwa na kwamba kuna umuhimu kwa watumishi kuhakikisha suala
hili linapewa umuhimu wa juu.
Alisisitiza suala la mahusiano kwa watumishi wa umma mahali pa kazi kwani
kufanya hivyo kutaboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi mkubwa katika
kuwatumikia wananchi.
Aidha, alizitaka halmashauri kuratibu vizuri suala la wafanyabiashara
wadogo maarufu wamachinga ili wapewe maeneo ya kufanyia biashara zao bila
usumbufu.
Awali Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri
ya Wilaya ya Singida linalojengwa Ilongero katika Kijiji cha Mwahango kwa
thamani ya Sh.2.7 bilioni.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo,alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Singida, Ester Chaula, kuisimamia idara ya manunuzi ili ujenzi wa
jengo hilo uweze kukamilika na kuanza kutumika.
"Nimeridhishwa na ujenzi unavyoendelea, DED (Mkurugenzi wa
Halmashauri) isimamie idara ya manunuzi, wasikuvuruge, mkandarasi alipwe fedha
zake, " alisema.
Akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida inayojengwa kwa Sh.bilioni 19.5 Waziri Mkuu, alisema ujenzi wa hospitali hiyo itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa huu na mikoa jirani.
Post A Comment: