Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake ma Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis akihutubia wananchi  waliohudhuria kwenye Wiki ya Unyonyeshaji Duniani Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Naibu Waziri Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na mmoja wa akinamama wanaonyonyesha wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani. Kulia kwake ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida Dk Victorina Ludovick

Baadhi ya akinamama wakiwa na watoto wao wakisherehekea Maadimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida hivi karibuni.

 

Na Abby Nkungu, Singida

 

SERIKALI imeahidi kuendelea kutenga fedha zaidi na kusimamia utekelezaji wa miongozo, kanuni na sheria juu ya unyonyeshaji wa watoto maziwa ya mama ili kulinda  afya na ustawi wa kundi hilo katika jamii.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Mwanaidi Ali Khamis wakati akizungumza kwenye  uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya unyonyeshaji  Duniani yanayofanyika Kitaifa katika halmsahuri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Naibu Waziri huyo alisema kuwa lengo la hatua hiyo ya Serikali ni kuhakikisha watoto wote wananyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi na kutochanganyiwa chakula chochote ndani ya miezi sita ya awali kama inavyoshauriwa na wataalamu ili kulinda afya zao.

“Hivi sasa ni asilimia 43 tu ya watoto ndio wanaonyonyeshwa  hadi kipindi cha miaka miwili  na kuendelea  huku takwimu zikionesha asilimia 57 tu ya watoto ndiyo hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kuchanganyiwa na chakula kingine chochote wala kunyweshwa maji kwa kipindi cha miezi sita” alisema.

Kutokana na hali hiyo alisema pamoja na kutenga fedha, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo juu ya umuhimu wa akinamama wanaojifungua kunyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi na kunyonyeshwa ziwa pekee bila kuwachanganyia na chakula wala maji kwa miezi sita ili kujenga msingi imara wa afya na uhai wa mtoto.

"Unyonyeshaji watoto maziwa ya mama huzuia aina zote za utapiamlo na kuwepo uhakika wa chakula kwa watoto wachanga na wadogo" alisema na kuongeza;

Unyonyeshaji maziwa ya mama ni msingi wa maisha; hivyo kulinda, kuendeleza na kuimarisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto ni jambo lenye umuhimu katika kujenga Dunia na Tanzania endelevu".

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Lishe nchini, Dk Germana Leyna alibainisha kuwa upo uwezekano wa kuepuka unene na uzito usiofaa kwa asilimia 25 pindi mtoto anapokuwa mtu mzima iwapo mama atakuwa amemnyonyesha kikamilifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo.

Nao wadau wengine wa masuala ya afya na lishe, wanasema kuwa kauli hiyo juu ya kusimamia unyonyeshaji imekuja muda muafaka wakati wa utekelezaji wa Programu Juimuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iliyoanza mwaka 2021 na kuendelea hadi mwaka 2025.

“Kikubwa ni wadau kuendelea kushirikiana chini ya Programu hii inayoshughulika na masuala mtambuka ya watoto kuanzia umri wa miaka 0 hadi 8 ili kutoa elimu kwa jamii juu  ya umuhimu wa unyonyeshaji watoto wa maziwa ya mama”alisema Afisa Lishe katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Agness John na kuongeza kuwa;

“Hivi sasa kuna mtindo wa baadhi ya akinababa kunyonya maziwa ya mama badala ya kumwachia mtoto eti wakidai kuwa hiyo ni dawa ya kutoa "hangover" ya pombe suala ambalo alisema linapaswa kukemewa na kupigwa vita kwa nguvu zote kwani linamnyima haki mtoto" alisema na kuungwa mkono na Muuguzi Mkuu Mkoa wa Singida Yasinta Alute ambaye alisema suala la wanaume kunyonya maziwa ya mtoto limeanza kuota mizizi na linapaswa kukomeshwa mara moja.

“Sio suala la kumaliza maziwa ya mtoto tu lakini pia lazima utambue kuwa mtu mzima anaweza kuwa na maradhi na huenda ziwa hata halisafishwi na mtoto akija kunyonya ziwa hilo hilo, huoni kama kuna hatari ya kumwambukiza mtoto maradhi?.... akina baba acheni hizo” alisema kwa msisitizo.

Maadhimisho ya Wiki ya unyonyeshaji Duniani ni utekelezaji wa Azimio la Innocent, Italia la mwaka 1991 ambapo mwaka huu yameongozwa na Kauli mbiu inasemayo “Chukua hatua, endeleza unyonyeshaji: Elimisha na toa Msaada" lengo likiwa ni kulinda, kuhimiza na kuendeleza unyonyeshaji watoto maziwa ya mama kwa ajili ya afya na ustawi wa kundi hilo muhimu. 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: