Na Zainabu Ally/MOROGORO

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa ametoa rai kwa Jeshi la uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kutumia rasilimali za Hifadhi kibiashara ili kuongeza idadi ya watalii na kuchagiza ongezeko la mapato kupitia sekta ya Utalii.

Mhe. Fatma Mwassa ametoa rai hiyo leo Agosti 14,2022 alipofanya ziara ya kikazi kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo hifadhini ikiwa ni mpango kuangalia utekelezaji wa maelekezo mbalimbali ya serikali kuhusu uimarishaji wa shughuli za uhifadhi na uboreshaji huduma za utalii.

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha miundombinu ya utalii sambamba na kuimarisha shughuli za uhifadhi wa maliasili kwenye Hifadhi za Taifa.

‘’Kama ambavyo mnafahamu utalii ni kipaumbele kwa nchi, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameamua kuwekeza zaidi kwenye utalii ili kuongeza mapato zaidi, tunatakiwa kuendelea kufanya biashara ya utalii wenye tija ili kuongeza pato la taifa’’ Alisema Mhe Fatma Mwassa.

Aidha, Mhe. Fatma Mwassa alisema kuwa Serikali ya mkoa inaunga mkono shughuli mbalimbali zinazofanywa na Hifadhi ikiwa pamoja na kupambana na kudhibiti ujangiri ambapo amewataka Hifadhi Taifa ya Mikumi na Kanda ya Mashariki kuendelea kupambana na kudhibiti ujangiri na uharibifu wa mazingira.

‘’Hatuwezi kuruhusu ujangiri katika mkoa huu. Tunatakiwa kuweka mikakati madhubutu kukabiliana na changamoto hii. Tusilegeze kamba hata kidogo kwa sababu na jangiri wanaoua wanyamapori ndio haohao wanaua hata watu. Hivyo, wasipewe mwanya. Serikali ipo pamoja nanyi kuukabili ujangiri na uharibifu wa mazingira ndani na nje ya hifadhi.

 Kwa bahati nzuri Mkoa wa Morogoro tumepata Katibu Tawala ambaye ni mtaalam na mbobezi katika masuala ya polisi jamii. Tunaamini kwa kutumia uwezo wake na utaalam wake tutafanikiwa kudhibiti ujangiri na uhalifu mwingine’’ Alisema Mhe. Fatma Mwassa.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Mikumi kuendelea kujitangaza zaidi na kwa kuweka bajeti maalumu ili kuongeza idadi ya watalii na mapato. Alishauri kujitangaza kupitia majarida na tovuti za mitandao ya kijamii ili jamii iweze kutambua vivutio vilivyo hifadhini na pia kujua maendeleo makubwa ya uboreshaji miundombinu ya Barabara, kiwanja cha ndege na maeneo ya malazi ya gharama nafuu iliyo ndani ya Hifadhi hiyo.

‘’Kwenye suala zima la biashara ni lazima tujitangaze. Maendeleo yaliopo sasa katika Hifadhi ni makubwa sana lazima wananchi wayatambue, wakati tunayafanya haya kwenye hii idara yenu ya mahusiano vitu vyote vinanyofanywa hapa hakikisheni vimeandaliwa kwa namna bora ya kuwavutia watalii kwa kufanya maandalizi bora ili kukuza soko la utalii wa kibiashara’’ Alisema Mhe. Fatma Mwassa

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda ya Mashariki Kamishna Msaidizi Mwandamizi Massana Mwishawa akaeleza kuhusu mikakati ya kudhibiti ujangiri ndani na nje ya hifadhi, kuendeleza mahusiano kati ya hifadhi na jamii pamoja na kuendelea kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwenye soko la ndani na nje ya nchi kwa kutangaza vivutio vya asili, malikale na tamaduni za watanzania kwa kule ya zaidi vivutio vilivyo kwenye mkoa wa Morogoro.

“TANAPA tumejipanga vizuri kupambana na kudhibiti ujangiri. Tunatekeleza hilo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na pia kuendelea kushirikiana na ofisi yako. Vile vile, tutaendelea kuboresha mahusiano na jamii sambamba na kuendelea kutangaza vivutio vilivyo kwenye Hifadhi ya Mikumi.

 Kwa utalii wa ndani, tutaelekeza nguvu zaidi kwa watalii wa ndani hasa makundi ya wananchi, wafanyabiara na wanafunzi wa mashule na vyuo kwenye mkoa wa Morogoro, DAR es Salaam na mikoa mingine ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi ya Mikumi pamoja na hifadhi zingine za Kanda ya Mashariki. Hili tutalifanya kwa kushirikiana na wadau hasa sekta binafsi. Malengo yetu ni kuing’arisha Hifadhi hii zaidi hatimae iwe na mchango mkubwa kwenye pato la taifa” Alisema Massana Mwishawa

Serikali ya awamu ya sita imejidhatiti kuboresha sekta ya utalii nchini kwa kuboresha miundombinu ili kuzifanya Hifadhi za Taifa nchini ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kuweza kufikika na kuzifanya Hifadhi ziweze kuongeza mapato.
Share To:

Post A Comment: