Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewahakikishia wananchi wa Msomera wilayani Handeni kuwa huduma ya maji itapatikana kwa muda wote. Amesema, visima vya maji vilivyochimbwa vinauwezo wa kuhudumia zaidi ya  mahitaji ya maji ya wakazi wa eneo hilo na kazi ya uchimbaji wa bwawa na ujenzi wa miundombinu ya maji inaendelea ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na  huduma ya maji karibu na makazi yake. 


Mheshimiwa Mahundi ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi wilayani hapo wakati akikagua utekelezaji wa mradi wa huduma ya majisafi katika kijiji cha Msomera chenye wakazi waliohamia kwa hiari  kutoka Ngorongoro. 


Aidha, amemuagiza Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo kuhakikisha anamsimamia mkandarasi ili ndani ya siku saba tenki kubwa lenye ujazo wa lita 167,000 liwe limekamilika na kupokea maji kwa ajili ya kusambaza kwa wananchi.


Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Siriel Mchembe ameipongeza Wizara ya Maji kwa juhudi inazofanya ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Handeni. Amesema utekelezaji wa haraka wa huduma ya maji hasa katika eneo la Msomera inadhihirisha nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kuhakikisha anatatua changamoto za huduma ya maji kwa Watanzania. Amewataka wananchi wa Msomera kutumia maji katika shughuli za kiuchumi. 


Amesema msisitizo wa serikali ni kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi na huduma ya maji  kwa kuanzisha kilimo cha kisasa ambapo Mbunge wa eneo hilo Mhe.John Sallu amewataka wananchi wote wenye utayari wa kuhama kutoka Ngorongoro kujitokeza kwa hiari.


Kwa upande wao wananchi waliohama kwa hiyari kutoka Ngorongoro wameipongeza serikali kwa uamuzi huo. Wamesema hawajutiii kuhama kwani serikali katika eneo la Msomera imewawekea mazingira mazuri ya kunufaika na ardhi na rasilimali zinazopatikana eneo hilo.


Mmoja wa wakazi hao Mzee Samwel Daniel ambaye pia ni Mwenyekiti wa jamii hiyo amesema ameiona fursa ya kilimo hivyo ameanzisha kilimo cha mbogamboga ambacho wananchi wenzake wanaweza kujifunza kama shamba darasa. Amesema fursa ya kufanikiwa ni kubwa kutokana na uhakika wa upatikanaji wa maji.






Share To:

Post A Comment: