Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe leo tarehe 23 Julai, 2022 amezindua shamba la kwanza lenye ukubwa wa ekari 11,453 kwa ajili ya Mradi wa Vijana wa mashamba ya pamoja (Block Farm) katika vijiji vya Mlazo na Ndogoe katika Halmashauri ya wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.


Waziri Bashe amesema shamba la pamoja (Block Farm) la kijiji cha Mlazo na Ndogoe ni la kwanza kuzinduliwa na kuongeza kuwa shamba ya pili la Bahi yenye ukubwa wa ekari 3,560 ni maalum kwa kilimo cha ngano; Lipo Halmashauri ya wilaya ya Bahi na shamba la tatu ni la Membe lenye ukubwa wa ekari 8,000 ambalo lipo katika Halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. 


Waziri Bashe amezindua shamba hilo kuashiria kuanza kwa hatua ya awali ya kulisafisha pamoja na kuweka miundombinu muhimu kwenye eneo hilo ikiwemo kutenga eneo la kilimo, ambalo limegawanywa kwenye mashamba madogo yenye ukubwa wa ekari 2,500.


Kazi nyingine ni uchimbaji wa visima na mabwawa ambapo kazi hiyo itafanywa kwa pamoja kati ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC).


Waziri Bashe ameongeza kuwa kazi nyingine ni kutenga na kujenga eneo maalum kwa ajili ya kujenga makazi ya Vijana, watakaoshiriki kwenye shughuli za kilimo pamoja na ujenzi wa eneo maalum la malisho ya mifugo na mahali kwa ajili ya maji ya mifugo na majosho.


“Wekeni pia eneo la Wenyeji ambao ni Wafugaji, watalisha na kunywesha mifugo yao, wekeni pia eneo maalum kwa ajili ya Wakulima wa hapa ili na wao wawe sehemu ya Mradi huu.” Amesisitiza Waziri Bashe.


Wakati huo huo; Waziri Bashe ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kuja kuuzindua rasmi Mradi wa shamba la pamoja (Block Farm) baada ya kukamilika kwake na kuongeza kuwa kila Mtaalam ambaye anawajibika katika Mradi huo, kuhakikisha kazi inafanyika na inakamilika ifikiapo mwezi, Machi, 2023.


Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Mlazo, Bwana Gallus Mahundi amesema Mradi wa mashamba ya pamoja umepokelewa vizuri na Wanakijiji na kuongeza kuwa Wananchi wapo tayari kushiriki moja kwa moja kama Wakulima na wakati huo huo watakuwa na uhakika wa soko la mazao watakayolima.


Mwenyekiti wa kijiji cha Ndogoe, Bwana Haruni Mahundi amesema, awali Wanakijiji hawakuwa wamepewa elimu ya kutosha kuhusu manufaa ya Mradi wa kilimo cha mashamba ya pamoja (Block Farms).


“Kwa sasa wameuelewa Mradi na wameahidi, kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji wa mazao ya kilimo na tunataraji kupata ajira kutokana na uwepo wa Mradi huu”. Amekaririwa Bwana Haruni Mahudi.


Naye Diwani wa Kata ya Nghambaku, Bwana Haruni Siengo amesema hakuwahi kufikiria kama kuna siku angeona aina hiyo ya Mradi wa kilimo cha mashamba makubwa na ya pamoja (Block Farms) na kuongeza kuwa wakati Halmashauri ya wilaya ya Chamwino ilipoleta ombi la eneo, walikubali mara moja kulitoa eneo hilo.

Share To:

Post A Comment: