Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo, akizungumza na Wakufunzi wa Makarani wa Sensa ya Watu na Makazi baada ya kuhitimu mafunzo hivi karibuni yaliyofanyika Chuo cha Ufundi VETA mkoani hapa.
Mtoto kama huyu mwenye Ualbino anastahili kuandikishwa ili aweze kufahamika na mahitaji yake ya msingi_ ikiwemo elimu, miundombinu na zana za kujifunzia viweze kuandaliwa na Serikali.

 Watoto walemavu kama hawa wanatakiwa kuandikishwa wakati wsa Sensa ya Watu na Makazi ili Serikali iweze kujipanga kwa ajili ya mahitaji yao ya msingi_ ikiwemo elimu na afya......

 

Na Abby Nkungu,  Singida

 

WAZAZI wa watoto wenye ulemavu wametakiwa kuhakikisha kuwa kundi hilo linahesabiwa wakati wa Sensa ya Watu na Makazi ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kuandaa mipango ya kibajeti, Sera, Sheria, Kanuni na Programu zitakazojibu changamoto zao.

Mwito huo ulitolewa na  Mratibu wa  Sensa ya  watu  na Makazi mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo wakati akizungumzia maandalizi ya zoezi hilo lililopangwa kufanyika kote nchini Agosti 23, mwaka huu.

Alisema kuwa wakati Serikali ikitekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya miaka mitano juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iliyoanza mwaka jana, takwimu sahihi za kundi hilo ni muhimu sana katika kufanikisha mipango mbalimbali ya watoto iliyowekwa.

“Programu hii inashughulika na masuala mtambuka ya watoto kuanzia umri wa miaka 0 hadi 8; wakiwemo watoto wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi wao kuhakikisha wanahesabiwa na kueleza bayana bila kificho hali zao”  alisisiza Kipuyo.

Alisema kuwa  ni vyema  wazazi na walezi  wakatambua kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya takwimu sura 351, hivyo iwapo mtu atamficha mtoto wake au yeye mwenyewe kukataa kuhesabiwa anaweza kushitakiwa chini ya  kifungu 6 (2) a cha sheria hiyo.

Alisema, kwa upande wake Serikali imejipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo muhimu kwa Taifa linafanikiwa bila kikwazo chochote kwa kuunda kamati za sensa hadi ngazi ya kitongoji na mitaa kwa ajili ya kutoa elimu na hamasa ili kila mwananchi aweze kujitokeza kuhesabiwa.

Hata hivyo, mmoja wa wazazi Patrick Mdachi mkazi wa Mitunduruni Manispaa ya Singida alisema kuwa pamoja na  maandalizi mazuri yaliyofanyika, bado kuna haja ya elimu na hamasa zaidi ili kuondoa dhana  na imani potofu kwa  baadhi ya jamii juu ya watoto wenye ulemavu katika kuhesabiwa.

“Mpaka sasa bado shule zenye watoto wenye mahitaji maalum zinapata changamoto kubwa kupata wanafunzi, baadhi wanafichwa majumbani na  wengine wanaandikishwa wakiwa na umri mkubwa. Ipo haja ya elimu na hamasa zaidi kwa kutumia wazee wa mila, viongozi wa dini, vitongoji, mitaa na wengine wenye ushawishi" alieleza.

Kauli ya Mdachi inaungwa mkono na Mwalimu wa kitengo cha Elimu Maalum shule ya msingi Mchanganyiko Mgori katika halmashauri ya wilaya ya Singida, Hemed Kilango ambaye anasema wazazi wengi wenye watoto walio na mahitaji maalum wamekuwa wakisita kuwapeleka watoto wao shule kwa kuhofia watateseka zaidi kutokana na kukosekana miundombinu ya kutosha huko.

“Kama wanawaficha kwenda shule, ni dhahiri hata sensa wanaweza kuwaficha,  hivyo ni lazima wazazi na walezi wakaelimishwa ipasavyo ili watambue kuwa mipango ya vifaa vya kutosha kujifunzia na kufundishia na miundombinu rafiki kwa watoto wenye ulemavu inategemea sana takwimu sahihi za sensa” alifafanua Mtaalamu huyo wa elimu maalum.

Naye, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Tumaini Viziwi ya mjini Singida, Francis Edward alieleza kuwa wamekuwa wakipokea idadi ndogo ya wanafunzi kutokana na wazazi kuwaficha watoto wenye mahitaji maalum wakidhani kwa kufanya hivyo watajiaibisha au kujifedhehesha.

Kulingana na ratiba ya maandalizi ya zoezi hilo, mafunzo ya wakufunzi wa sensa ngazi ya mkoa  Singida yamehitimishwa juzi ambapo yatafuatiwa na mafunzo mengine katika halmashauri zote  saba hapo kesho yatakayohusisha  makarani na wasimamizi zaidi ya  15,400.


Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: