Mkuu wa Kitengo Cha Ukuzaji Biashara na Masoko wa Benki ya Mwalimu (MCB), Bi.Leticia Ndongole akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam Baadhi ya wananchi wakipata huduma kwenye banda la Mwalimu Benki mara baada ya kutembelea banda hilo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam Watumishi wa Mwalimu Benki wakipata picha ya pamoja katika banda lao kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam

****************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WANANCHI wameendelea kutembelea banda la Mwalimu Benki katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam ambapo mpaka sasa wameshawahudumia watanzania 50 waliotembelea banda hilo.

Akizungumza katika maonesho hayo leo Julai 7,2022 Mkuu wa Kitengo Cha Ukuzaji Biashara na Masoko wa Benki ya Mwalimu (MCB), Bi.Leticia Ndongole amesema wanatarajia idadi ya wakopaji na wateja wapya itaongezeka kwa kuwa huduma zinatolewa kwa watu wote.

“Tunaposema huduma tunatoa kwa watu wote maana yake ni walimu, wafanyabiashara, wanafunzi wa vyuo, wakulima, wafugaji, wasafirishaji, vijana na wazee... hatuachi mtu. Tunafungua akaunti za aina mbalimbali kwa hapa tumefungua akaunti 35 hivyo tunawakaribisha wote kuja kupata huduma zetu bora kwenye sekta ya benki". Amesema Bi.Leticia.

Aidha Bi.Leticia amesema wanatoa huduma kwenye mikoa yote hapa nchini kwenye matawi na kidijitali kupitia mawakala wa Mwalimu Benki, Mwalimu Mobile na Mwalimu Visa Card pia wateja wao hupata huduma zote za bima na mikopo ya vifaa mbalimbali vya ujenzi.

Pamoja na hayo amewakaribisha wananchi kwa ujumla kutembelea banda lao kwaajili ya kupata huduma za kibenki hasa mikopo ambayo itawasaidia kujiinua kiuchumi binafsi na taifa kwa ujumla.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: