MOSHI

Mbunge wa jimbo hilo Prof. Patrick  Ndakidemi amewataka  wanavikundi kuwa na mchanganyiko wa viongozi  kutoka jinsia zote  wenye kuweza kutetea katiba ya kikundi  na watakaozingatia sheria, taratibu na kanuni za kikundi cha ili viweze kuwa endelevu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa  kikundi cha wajasiriamali wadogo cha 'HAPA KAZI GROUP kilichopo katika kijiji cha Kirima Juu kata ya Kibosho Kirima Mbunge huyo alisema vikundi viingi  vinashindwa kufikia malengo kutokana na safu za uongozi wanazoweka ambazo zinakuwa upande mmoja.


'Naomba muone umuhimu wa kuchanganya watu wa jinsia zote kwenye uongozi wenu lengo ni kuwa mtaweza kusonga mbele zaidi ya sasa lakini pia ni kuweka mawazo mbadala kuliko kubaki na mawazo ya upande mmoja pekee"alisema


Aidha Prof .Ndakidemi  aliwapongeza kwa hatua waliyochukua ya kuanzisha kikundi chenye lengo la kuwaingizia kipato sanjari na kujikwamua na umaskini na kuwa  kupitia shughuli za kikundi wanachama wataweza kuimarisha vipato vyao na kuchochea maendeleo ya familia na kuboresha lishe zao.


Alisema  kuwa faida ingine kubwa ya kuwa kwenye kikundi ni kwamba itakuwa rahisi kuwashawishi wataalamu wa fani mbalimbali kuja kutoa huduma za mafunzo kwa kikundi cha watu wengi kuliko kwa mtu mmoja.


Kuhusiana na changamoto ya eneo la kulima, Prof Ndakidemi aliwashauri wawasiliane na uongozi wa shamba la vyama vya ushirika vya KIMASIO na Kirima Boro ili wakodishe shamba na kutekeleza miradi ya kilimo cha mbogamboga ambacho kitakuwa na manufaa kwa wanakikundi hao 


"Naomba na mimi niwaunge mkono kwa hizi jitihada mlizozionyesha katika kupambana au kujikwamua kiuchumi na naomba niwaunge mkono kwa kuwachangia milioni moja ili kutunisha kidogo mfuko wetu huu"alisema


Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi  mwenyekiti wa kikundi hicho  Vincent Shio alieleza kuwa kikundi hicho chenye wanachama 38 wa jinsia tofauti kimeanzishwa kwa lengo la kuwaweka pamoja na kujishughulisha na shughuli za kilimo, ufugaji na kufanya biashara ndogo ndogo. Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ni kuwa  hadi kikundi kilipozinduliwa  kimefanikiwa kukusanya michango kutoka kwa wanachama ambapo wameweka kiasi cha shilingi laki saba benki. 


"Mheshimiwa mbunge ni kiwa kila jumapili wanakikundi huwa tukutana na kutoa mchango wa shilingi elfu moja kutoka kwa kila mwanachama na kujadili mipango na maendeleo ya kikundi chetu hiki"alisema


 Kadhalika mwenyekiti huyo alisema  changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa eneo la kutekeleza miradi ya kilimo na mtaji mdogo wa kuendesha shughuli za miradi yao ya kilimo, ufugaji na biashara.Share To:

JUSLINE

Post A Comment: