Na Mwandishi Wetu


Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI imelenga kupunguza vifo vya Wajawazito na watoto kupitia mikataba itakayobeba viashiria vya Wajawazito na lishe inayotarajiwa kusainiwa na Wakuu wa Mikoa. 


Dkt. Sichalwe ameyasema hayo katika kikao cha Wadau wa Sekta ya Afya kwenye eneo la mama na mtoto pamoja na Lishe kilichofanyika Mkoani Singida.
“Tumekubaliana kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais aliyoyatoa ya kuja na mkataba mmoja ambao utakuwa umebeba viashiria vya utendaji vya akina mama wajawazito pamoja na masuala ya Lishe ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupambana dhidi ya vifo vya Wajawazito na watoto wachanga”.Amesema Dkt. Sichalwe 
Aidha amesema kuwa, pamoja na hayo Serikali kwa kushirikiana na wadau imekubaliana kuanza kutekeleza matumizi ya kanzi data, yatakayotoa fursa ya kujua viashiria vya hatari vya mjamzito endapo anavyo kutokana na maswali atayoulizwa na Mtaalamu wa afya.


Sambamba na hilo Dkt. Sichalwe amesema, kwa upande mwingine Serikali kwa kushirikiana na wadau wamekubaliana utekelezaji wa azimio la vikao vya kujadili vifo vya mama na mtoto vilivyoanzishwa na Wizara ya Afya kikanda. 
Aidha, Dkt. Sichalwe ameeleza kuwa, kwa pamoja kama Wadau wa Sekta ya Afya wamekubaliana kutekeleza mfumo wa kusimamia magari ya kubebea Wajawazito (M-MAM) unaorahisisha mfumo wa rufaa nchini kama sehemu nyingine ya mkakati wa kupambana dhidi ya changamoto ya vifo vya Wajawazito na watoto. 


Mbali na hayo, Dkt. Sichalwe amewashukuru Wadau waliojitokeza katika kikao hicho cha Kimkakati na kuweka wazi kuwa, maazimio yote ya kikao hicho yatawasilishwa kwenye uongozi wa Wizara ya Afya na TAMISEMI kwaajili ya utekelezaji na Wadau wote walioshiriki kikao hicho na wasio shiriki watakuwa katika utekelezaji. 
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, wamekubaliana kuleta mipango yao, namna walivyotekeleza na changamoto wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa mipango hiyo na wanaishauri nini Serikali ili kwa pamoja kuona namna gani wanaweza kushirikiana kuzitatua kwa lengo la kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya mama na mtoto katika jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema, katika kikao hicho wamepitia viashiria mbalimbali vinavyolenga masuala ya mama na mtoto ambavyo vitasaidia kuongeza uwajibikaji kwa viongozi mbalimbali ngazi ya Mkoa na kupima matokeo ya uwajibikaji huo kwa kupungua kwa vifo vya Wajawazito na watoto. 


Pia, Dkt. Kapologwe amesema kuwa, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ambapo vituo vya afya 650  ambavyo vinatoa huduma za upasuaji vimejengwa, huku hospitali mpya za Halmashauri 130 zikijengwa, hivyo uwekezaji huo ni lazima uende sambamba na huduma bora zitazosaidia kupungua kwa vifo vya Wajawazito na watoto. 
“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu, katika kipindi cha miaka mitano vituo vya afya 650 vinavyotoa huduma za upasuaji, sambamba na hilo hospitali mpya za Halmashauri 130, sasa uwekezaji huo lazima uende sambamba na huduma.” Amesema Dkt. Kapologwe

Share To:

Adery Masta

Post A Comment: