Moses Mashalla,


Sakata la gari lililoshikiliwa kwa tuhuma za kubeba madawa ya kulevya limeibuka tena ndani ya kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Jiji la Arusha kilichofanyika leo katika ukumbi wa jiji.


Gari hilo lenye nambari STJ 7333 lilishikiliwa mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu na jeshi la polisi wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro likiwa na shehena ya mirungi ambapo linashikiliwa mpaka sasa.


Akiibua hoja hiyo ndani ya kikao hicho diwani wa kata ya Ngarenaro,Isaya Doita aliuliza nini hatma ya gari hilo ambalo lilikamatwa likiwa na shehena ya mirungi.


“Mheshimiwa Mwenyekiti gari hili mpaka sasa linashikiliwa na hatujui linarejeshwa lini tunaomba kupata ufafanuzi “alisema Doita 


Akijibu swali hilo afisa utumishi wa jiji la Arusha,Gerald Ruzika alisema kuwa mpaka sasa gari hilo bado linashikiliwa na polisi wilayani Rombo kama kielelezo na derava wake yuko rumande na kuwataka madiwani waendelee kuwa na subira.


Katika hatua nyingine Meya wa jiji la Arusha,Maximillan Iranqe alifafanua suala la uwekaji wa taa za barabarani pembezoni mwa hoteli yenye hadhi ya nyota 5 ya Grand Melia na kusema kuwa tayari maandalizi ya uwekaji wa taa hizo yanaendelea.


Meya huyo alifafanua kuwa jiji la Arusha kwa kushirikiana na uongozi wa hoteli hiyo wanatarajia kuweka taa hizo pembezoni mwa barabara inayopita hotelini hapo kwa lengo la kuimarisha usalama.


“Grand Melia ni hoteli yenye hadhi ya nyota 5 lazima tuipe kipaumbele hivyo tutashirikiana nao kwa kuweka taa hizo kuimarisha usalama “alisema Meya Iranqe 


Share To:

Post A Comment: