Jenereta maalum ikishushwa Kituo cha Afya Mkumbara kilichopo wilayani Korogwe, mkoani Tanga baada ya kupokea vifaa hivyo vilivyonunuliwa na serikali kupitia Bohari ya Dawa MSD.Jenereta maalum pamoja na baadhi ya vifaa tiba vilivyonunuliwa na serikali vikishushwa katika Kituo cha Afya cha Majengo, wilayani Korogwe.Vifaa hivi ni kwa ajili ya kuboresha huduma za dharula kwa mama wajawazito na watoto (CEMONC)

***********************

NA MWANDISHI WETU



WANANCHI wa eneo la Mkumbara wilayani Korogwe mkoani Tanga wameishukuru serikali kwa hatua zilizochukuliwa za kununua vifaa vya kisasa vya huduma ya mama na mtoto ambavyo vitasaidia kuokoa maisha ya wajawazito wanaokabiliwa na changamoto za uzazi na kuhitaji kufanyiwa upasuaji.

Wamesema, katika kijiji hicho kwa muda mrefu kituo cha afya kilikuwa hakina jenereta hivyo inapotokea hitilafu ya umeme huweza kuhatarisha utoaji huduma kwa wagonjwa wanaokuwepo kituoni hapo.

Akizungumza katika kijiji hicho mkoani Korogwe, Mwenyekiti wa Kamati ya afya ya kijiji Rajabu Dassa, alisema wanaishukuru serikali kwa kuboresha huduma za afya katika kijiji hicho hususani za wanawake na watoto kwa kuwa awali walikuwa wakitembea umbali wa kilometa 21 kufuata huduma hizo,hasa za upasuaji.

Dassa ameongeza kuwa,mbali na jenereta walilopokea, huduma ya vifaa tiba hususani vya maabara na dawa pia imekuwa ya uhakika.

Aliiomba serikali, kuendelea kuboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa wodi za wanawake na wanaume, kwa kuwa kwa sasa hazitoshelezi uhitaji.

Naye Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dkt.Peter Mfumya, alisema kituo hicho kinahudumia kata sita ikiwemo ya Mazinde, Mkumbara, Mkomazi,Bendera, Hedaru na Ndunga.

Alisema awali kabla ya kuja kwa jenereta hilo na vifaa vya kisasa walikuwa wakifanya upasuaji hususani kwa wajawazito kwa kutegemea umeme wa Shirika la TANESCO pekee na inapotokea hitilafu, vifaa husika vilihifadhi umeme kwa saa tatu tu kabla ya kuzimika.

"Hapa watu wanaohitaji huduma ya upasuaji ni wengi hususani wajawazito ikitokea umeme umekatika, vifaa vinahifadhi nishati hiyo kwa saa tatu tu, kama hamjamaliza ndio hatari hivyo hutulazimu kufanya haraka haraka ili isitokee shida,"alisema.

Alisema kwa siku wanahudumia wagonjwa 100, hivyo wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza watoa huduma katika ajira mpya za hivi karibuni kwa kuwa awali walikuwa 10 na sasa wataongeza saba, hali itakayowezesha kuwa na muda wa kupumzika.

Pia Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Korogwe Mji Dkt.Salma Suedi alisema awali walikuwa wakitumia jenereta ndogo ambalo halina uwezo wa kutosha hivyo wanashukuru kuletwa kwa jingine jipya vifaa nakutengewa sh.bilioni 1.2 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya hospitali hiyo.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: