Serikali imejipanga kuzalisha miche ya kahawa milioni 20 kupitia wadau mbalimbali wakiwemo Bodi ya Kahawa, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI) na Sekta binafsi. 

Hayo yamesemwa leo tarehe 02 Julai, 2022 na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde alipotembelea Makao Makuu ya TaCRI yaliyopo kata ya Lyamungu, Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro. 


"Sote tunafahamu kuwa kahawa ni moja ya zao la kimkakati, hivyo Wizara tumeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wake ambapo hatua ya awali ni kuongeza uzalishaji wa miche bora ambayo ina ukinzani wa magonjwa na tija kubwa kwa wakulima.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameongeza bajeti ya Kilimo kutoka bilioni 294 hadi bilioni 954, ongezeko hilo si kwa bahati mbaya, ni kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele cha juu kuendeleza sekta ya kilimo nchini. Hivyo, ongezeko hilo la bajeti tumelipeleka kwenye vipaumbele vikiwemo kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, utafiti, kuimarisha huduma za ugani, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.


Naitaka TACRI pamoja na kuendelea kuongeza uzalishaji wa miche bora, lakini pia mjikite katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya miche hiyo na mbinu bora za kufuata ili waweze kuzalisha kahawa kwa tija na kuongeza kipato chao”Alisema Mavunde


Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa TACRI, Dkt. Deusdedith Kilambo, aliishukuru Serikali kwa kuongeza bajeti yao kutoka milioni 328 mwaka 2021/2022 hadi milioni 800 mwaka 2022/2022 na kusisitiza kwamba TaCRI wamejipanga kuhakisha lengo la kuzalisha miche bora milioni 20 kwa mwaka 2022/2023 linafikiwa.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai, Juma Irando alimhakikishia Naibu Waziri Mavunde kuwa Serikali ya Wilaya itatoa ushirikiano wa kila hali kwa TaCRI ili waweze kufikia lengo la kuzalisha miche milioni 20. Vilevile, aliongeza kuwa kama sehemu ya kuunga juhudi mkakati huo wa Serikali, Halmashauri ya Hai imepanga kuongeza vitalu vya miche ya kahawa ili kufikia mahitaji makubwa ya wakulima.

Share To:

Post A Comment: