MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana akizungumza kwenye kikao cha ndani cha Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana amemshauri Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camilius Wambura, kufanya tathimini ili kuona kama inawezekana kupunguza idadi ya askari wa usalama barabarani ambao wamekuwa wakilalamikiwa kusababisha kero kwa wananchi.


Kinana ametoa ushauri huo jana akiwa katika mwendelezo wa ziara yake katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo na kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya mikoa ya Songwe na Mbeya dhidi ya idadi kubwa ya askari wa barabarani ambao wamekuwa wakiwasimamisha mara kwa mara, hivyo kucheleshewesha shughuli za maendeleo.

Malalamiko hayo ya wananchi yaliendelea kuibuka hata kwenye kikao cha ndani cha Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe ambapo mmoja wa wanachama wa Chama hicho ambaye ni dereva wa magari ya kubeba abiria maarufu kama Costa, kutoa malalamiko yake mbele ya Kinana akidai wamechoka kusimamishwa mara kwa mara na matrafiki na kila wanaposimama wanatozwa Sh. 2000 kwa kila kituo.

Akijibu malalamiko hayo Kinana, alisema kwanza anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Wambura. “Nampongeza Rais kwa kumtea IGP mpya, nina hakika ni IGP mwadilifu, mchakazi na hodari.

“Lakini namuomba na kumshauri atizame wingi wa trafiki mijini, kila baada ya muda mfupi unasimamishwa na trafiki, wenye magari hawaendeshi kwa raha, hivyo nimsihi IGP afanye tathimini kuhusu uwepo wa trafiki wengi kwenye miji yetu, wamekuwa wengi sana kila ukitembea kidogo unasimamishwa, kilometa moja unakuta trafiki.

“Namuomba IGP afanye tathimini watu wapumue, watu biashara zao zinaharibika kwa sababu ya kuambiwa paki pembeni, tunaheshimu umuhimu wa usalama nchini, lakini tunakerwa na kuambiwa paki gari pembeni. Namuomba IGP, naheshimu na natambua uwezo wake mkubwa, lakini afanye tathimini, je, kuna umuhimu wa kuwa na idadi kubwa ya trafiki barabarani?” Alihoji Kinana.

Pamoja na hayo, Kinana alisema katika ziara yake amepokea malalamiko mengi ya wananchi wakilalamikia idadi ya trafiki na katika kushughulikia malalamiko hayo, ametoa ushauri kwa IGP Wambura kuangalia uwezekano wa kufanya tathimini kuhusu uwepo wa idadi ya trafiki barabarani.

Kwa upande wake IGP Wambura alipotafutwa na waandishi wa habari, alisema ushauri huo ni mzuri na atakwenda kuufanyia kazi ndani ya taasisi yake. ”Ushauri ulitolewa ni mzuri nimeusikia na nakwenda kuufanyia kazi ndani ya taasisi yetu.”

Wakati huo huo Juma Shaban ambaye ni dereva wa magari ya kubeba abiria kati ya Mkoa wa Songwe na Mbeya alisema ni vema kukawa na utaratibu mzuri utakaowekwa na trafiki wa kuwa na vituo maalumu vya kukaa barabarani badala ya kuwepo kila mahali kwani imekuwa kero kubwa na wakati mwigine inafanya kazi yao kuwa ngumu.
Share To:

Post A Comment: