Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda (katikati) akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo leo Julai 21, 2022 kuhusu hatua ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa wakati wa ziara yake wilayani humo mkoani Singida hivi karibuni baada ya wananchi kuonesha kero zao walizoziandika katika mabango wakilalamikia wajawazito kutozwa fedha wakati wa kujifungua Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi na mambo mengine. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora na kulia ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Pius Sangoma.
Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Pius Sangoma.akizungumza kwenye mkutano huo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora akizungumza kwenye mkutano huo.
Watumishi wa wilaya hiyo wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Taswira ya mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale, Iramba, Singida


WATUMISHI 20 wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida ambao ni kati ya 52 waliotuhumiwa kukusanya mapato zaidi ya Sh.Milioni 353 na kushindwa kuziingiza kwenye mfumo wa mapato wa halmashauri wameanza kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, watumishi wengine wanne wa Hospitali ya  Wilaya  Kiomboi nao wameingia matatani baada ya kubainika wamekuwa wakiwatoza fedha na kuwadai rushwa wajawazito wanaokwenda kujifungua katika hospitali hiyo.

Kuanza kuchukuliwa hatua watumishi hao kunafuatia agizo lililotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara wilayani humo Julai 16, mwaka huu na kubaini ufisadi wa fedha unaofanywa na baadhi ya watumishi wasiowaaminifu katika halmashauri hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, akizungunza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo leo Julai 21, 2022 ,  alisema baada ya maagizo ya Waziri Mkuu, kuliundwa kamati ya kuchunguza mambo kadhaa yaliyolalamikiwa na wananchi likiwamo suala la fedha hizo zilizokusanywa lakini hazikupelekwa benki.

Alisema katika uchunguzi huo imebainika watumishi 17 ambao ni kati ya 52 waliotuhumiwa mashtaka yao yamethibitika kwamba walikusanya mamilioni ya fedha lakini hawakuziingiza kwenye mfumo wa mapato ya halmashauri.

"Tunaziachia mamlaka zingine ziendelee na utaratibu wa kuwachukulia hatua na pia tunamwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya achukue hatua za kinidhamu," alisema.

Mwenda alisema watumishi wengine watatu ambao wamefunguliwa mashtaka ambayo yatarudiwa na taratibu za kurejea mashtaka hayo zifuatwe.

Aliongeza kuwa watumishi 13 kamati imebaini kuwa mashtaka yao hayajathibitika kutokana na kwamba fedha walizokuwa wakidaiwa walishazirudisha lakini madeni yao bado hayajaondolewa kwenye mfumo wa mapato wa halmashauri.

"Tunamwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri afuatilie ajiridhishe kama kweli watumishi hao wamelipa madeni hayo ili waondolewe kwenye orodha ya wadaiwa.

Mwenda alisema watumishi wengine watatu, walikataa kupokea barua ya kuitwa kwenye kamati ya uchunguzi.

" Namwagiza OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) watafutwe na kukamatwa mahali popote walipo na barua zao watakabidhiwa wakiwa chini ya ulinzi wa polisi," alisema.

Kuhusu watumishi wa sekta ya afya, alisema Kamati ya Uchunguzi imebaini walikuwa wakiwatoza fedha wajawazito,kuwaomba rushwa,nguo na huduma ya uchunguzi ya Ultrasound  na gharama nyingine kinyume cha utaratibu.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataja watumishi hao kuwa ni Mhoja Mpenda, Lisa Ngwesheni, Magreth Dilu na Peter Boniventure.

"Watumishi hao wamekuwa wakiwaomba rushwa na kuwalipisha wajawazito fedha kwa ajili ya huduma za kujifungua kikiwemo kipimo cha ultrasound," alisema.

Mwenda alisema watumishi hao hatua itakayochukuliwa dhidi yao ni kupewa onyo kali la kimaandishi kwa mujibu wa sheria ili wapate nafasi ya kujieleza na kujitetea juu ya tuhuma zinazowakabili.

Waziri Mkuu, Majaliwa alipofanya ziara wilayani Iramba Julai 16, mwaka huu, wananchi wa mji wa Misigiri waliandika mababgo kadhaa ya malalaniko yakiwemo yaliyohusu wajawazito kutozwa fedha katika Hospitali ya Wilaya Kiomboi.


 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: