Na. Richard Bagolele - Chato


Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi  amewataka wananchi wa kata ya Bwanga wanaopakana na Shamba la miti la Silayo kuwa makini na matapeli  wanaouza ardhi ambayo ni sehemu ya hifadhi pamoja na kuchukua mali za wananchi.


Mkuu wa Wilaya ametoa tahadhali hiyo leo tarehe 06.06.2022 wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Nyarututu kata ya Bwanga.


Mkuu wa Wilaya amesema amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo wakidai kutapeliwa na watu ambao wamewauzia ardhi ya hifadhi ya serikali.


"Tuachane kuuza ardhi ya hifadhi si maeneo yenu, ni ya mali ya serikali, kuna watu wengi wamekuja kwangu kulalamika wametapeliwa na wanataka kurudishiwa fedha zao, acheni kununua ardhi ya hifadhi.


Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Chato amesema kuna watu wamekuwa wakivaa sare za mgambo na kujitambulisha kuwa wametumwa na Serikali ambapo wamekuwa wakichukua mali za wananchi ikiwemo mazao, kuku, baiskeli.


Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi hao kuwa makini na watu wa aina hiyo na amewataka wananchi kutoa taarifa haraka kwenye ofisi za serikali.


"wananchi mnadanganywa sana, mtu anafika kwenu anachukua kuku, mazao, basikeli, anasema mimi nimetumwa na serikali, huo ni uongo, shirikianeni na  toeni taarifa za wizi huu" amesisitiza Mkuu wa Wilaya.


Mapema Mkuu wa Wilaya ameeleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita Wilayani ikiwemo ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda ya Chato ambapo zaidi ya shilingi bilioni 40 zimetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa ujenzi na vifaa tiba sambamba na Sekta ya elimu ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 5 zimeletwa hadi sasa.


Katika Mkutano huo wa kusikiliza kero Mkuu wa Wilaya aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri, na taasisi zingine za serikali ikiwemo TARURA,  RUWASA na TANESCO.


Share To:

Post A Comment: