Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  Mkoa wa Singida Mzalendo Widege akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Mei 25, 2022 ya kila ya robo ya mwaka inayohusu utendaji kazi wa taasisi hiyo katika maeneo matatu ambayo ni Uchunguzi, Elimu kwa Umma na Uzuiaji wa Vitendo vya Rushwa kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2022. Kulia ni Afisa wa TAKUKURU, Richard Balina.
Maafisa wa TAKUKURU wakiwa katika mkutano huo wa kutoa taarifa kwa Umma kupitia vyombo vya habari.
Mkutano huo ukiendelea.
Taarifa ikitolewa.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.



Na Dotto Mwaibale, Singida


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida katika kipindi cha Januari hadi Machi 2022 imekagua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Sh.4,478,011,237.00. 

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida Mzalendo Widege wakati akitoa taarifa ya kila ya robo ya mwaka inayohusu utendaji kazi wa taasisi hiyo katika maeneo matatu ambayo ni Uchunguzi, Elimu kwa Umma na Uzuiaji wa Vitendo vya Rushwa kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2022.

Alisema miradi ya Maendeleo iliyofanyiwa ufuatiliaji na kukaguliwa ni kumi na tatu ambayo ni ya Barabara chini ya TARURA ambayo ilikuwa saba yenye thamani ya Sh. 2,523,627,600.00, Elimu miradi miwili yenye thamani ya Sh.660,000,000 ,  Afya Miradi  Mitatu yenye thamani ya Shs. 799,383,637.00 na Maji mradi mradi mmoja wenye thamani ya Sh. 495,000,000.00. 

Alisema mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi hiyo ambayo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa, yameweza kufanyiwa kazi kwa kutoa elimu kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa iliyopo na kuimarisha usimamizi wa miradi kwa kusisitiza uzingatiaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma ili kupata miradi bora yenye kukidhi thamani ya fedha (Value for money).

Alisema katika Dawati la Uchunguzi kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2022 TAKUKURU Mkoa wa Singida ilipokea jumla ya malalamiko 100 ambapo taarifa 73 zilihusu vitendo vya rushwa na taarifa 27 hazikuhusu vitendo vya rushwa.

Alitaja mchanganuo wa malalamiko hayo 100 yaliyopokelewa kisekta kuwa ni TAMISEMI - 41, Elimu- 12, Ardhi- 12,  Afya - 9, Mahakama 6, Mazingira-3, Fedha- 3, Polisi - 2, Kampuni za Ulinzi - 2, Binafsi -2, Manunuzi – 2, Manunuzi na Utalii - 2, Kilimo -1, Manunuzi - 1, Maliasili - 1 na Nishati-01.

Alisema malalamiko 73 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na Malalamiko 27 ambayo yalibainika hayahusiani na rushwa walalamikaji walipewa ushauri.

Widege alisema katika kipindi husika, jumla ya kesi mbili  zilifunguliwa Mahakamani na kufanya jumla ya kesi zinazoendelea mahakamani kuwa kumi na tatu na kuwa katika kipindi cha Januari – Machi 2022, kesi moja ilitolewa uamuzi mahakamani na Jamhuri ilishindwa. 

Akizungumzia kuhusu Elimu kwa Umma alisema inafanyika ili kuielimisha jamii kuhusu madhara ya rushwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla na kuwa inafanyika kwa madhumuni ya kuipa jamii uelewa na hivyo kuihamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa. 

Alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida kupitia Dawati la Elimu kwa Umma imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali katika kuelimisha kwa kuwashirikisha wanajamii wa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana wa shule za Msingi, Sekondari, Vyuo, Watumishi wa Umma na jamii kwa ujumla. 

Pia TAKUKURU Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Chama cha SKAUTI Tanzania, imefanikiwa kuanzisha umoja unaojulikana kwa jina la TAKUKURU - SKAUTI (TAKUSKA) na kuwa kupitia umoja huo wameweza kufanya mikutano katika kuhamasisha wazazi waruhusu watoto wao kujiunga na TAKUSIKA, kumefanyika makambi ambayo yamewawezesha vijana kufahamu mambo mbalimbali yakiwemo maalifa mbalimbali ya kuzuia rushwa na mbinu mbalimbali ya skauti makambi hayo yamefanyika mkoa mzima wa Singida .

Widege aliongeza kuwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2022 jumla ya mikutano ya hadhara 48 imefanyika, semina 23  zimefanyika, klabu  za wapinga Rushwa 82 zimeimarishwa, makala 15 ziliandaliwa na vipindi vya Redio 03  vilirushwa kupitia Standard Radio FM ya mkoani Singida.

Akizungumzia Uzuiaji wa Vitendo vya Rushwa alisema ni jukumu moja wapo linalotekelezwa na TAKUKURU kwa madhumuni ya kuzuia athari ambazo jamii ingezipata kama vitendo vya rushwa vingeachwa vikatokea. 

Alisema ili kudhibiti mianya ya rushwa katika Idara mbalimbali, TAKUKURU Mkoa wa  Singida imefanya uchambuzi wa mifumo kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa katika mifumo mbali mbali ili kubaini mapungufu.

Alitaja baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni uchambuzi wa mfumo juu ya tathmini ya utendaji kazi wa Wakala wa huduma ya ununuzi serikalini (GPSA)-Singida, Uchambuzi wa Mfumo wa Utendaji kazi wa Wakala wa huduma za ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani hapa, Uchambuzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Mapato yanayotokana na Ushuru wa Madini ya Ujenzi Halmashauri za Wilaya Manyoni, Iramba na Mkalama.

Alitaja uchambuzi mwingine kuwa  ni Mfumo wa Ukusanyaji na Usimamizi wa Mapato yatokanayo na lesani za Biashara Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mfumo wa Uendeshaji wa kamati za Usuluhishi wa migogoro katika ngazi za vitongoji Halmashauri ya wilaya ya Iramba,mfumo wa Ununuzi na malipo ya mazao ya Pamba katika Halmashauri ya wilaya ya Iramba.

Alisema kupitia chambuzi hizo, TAKUKURU Mkoa wa Singida imefanya  warsha na wadau husika kujadili matokeo ya chambuzi hizo na kuwekeana maazimio ya namna bora ya kuondokana na mianya ya rushwa iliyobainishwa katika maeneo yao ya kazi.     

Alitaja Warsha zilizofanyika kuwa ni pamoja na Warsha ya  kujadili matokeo ya uchambuzi wa mfumo kubaini mianya ya rushwa katika utendaji wa mabaraza ya ardhi ya kata katika  Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na Warsha kujadili matokeo ya uchambuzi wa  mfumo kubaini mianya ya Rushwa ya ngono katika sekta ya  elimu- Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Aidha Widege alisema TAKUKURU imefanya kazi ya ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Maazimio ya warsha zilizoketi kujadili juu ya Usimamizi wa Mitihani katika Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC)-Singida, Udhibiti wa mianya katika mapato na Matumizi ya Serikali ya Wanafunzi (TIASO)-Singida, Mfumo wa  kamati za Usuluhishi wa   migogoro ngazi ya vitongoji katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.

Alisema ufuatiliaji huo umejiridhisha na hatua za utekelezaji wa makubaliano hayo umetekelezwa.

Alisema Mkakati wa utendaji kazi TAKUKURU Mkoa wa  Singida kwa robo ya nne ya mwaka 2021/2022 inayoanzia Aprili hadi Juni, 2022 ni kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa Mkoa wa Singida kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,kufanya uchunguzi pale itakapobainika kuwa katika ufuatiliaji huo wa matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa Mkoa wa Singida vitendo vya rushwa vimejitokeza na kuendelea na uelimishaji unaolenga kushirikisha jamii katika mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekeleza Mpango Kazi wa TAKUSKA. 

Alisemma TAKUKURU Mkoa wa Singida inatoa rai kwa wananchi wote kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya Rushwa na kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa kwa njia mbalimbali ikiwemo kufika Ofisi za TAKUKURU Mkoa na wilaya au kupiga simu namba 113 au kupiga simu kwa Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida kwa Namba 0738-150-208, kutumia TAKUKURU APP hasa kwa Rushwa za barabarani pale wanapobaini kutokea/kutaka kutokea kwa vitendo vya Rushwa, kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani.

Alisema Mkoa wa Singida, kama ilivyo kwa mikoa mingine, kumekuwepo na wimbi la watu wanaojifanya Maafisa wa TAKUKURU na kujipatia fedha kwa kuwahadaa kuwa wanaweza kuwasaidia kupata huduma au nafuu zozote kutoka mamlaka mbalimbali za Serikali. 

TAKUKURU Mkoa wa Singida inawataadharisha wale wote wanaowatapeli au wanaopanga kuwatapeli wananchi kwa kujifanya Maafisa wa TAKUKURU au vyombo vingine vya dola kuacha kwa sababu watakapobainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida Mzalendo Widege ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Siku ya Jumanne Agosti 23 mwaka huu.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: