Katibu Mkuu wizara ya Katiba na sheria ,Mary Makondo akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Jijini Arusha leo.


Wakili Mkuu wa serikali , Gabriel Malata akizungumza katika ufunguzi  wa mafunzo hayo jijini Arusha leo.

Na Ahmed Mahmoud

KATIBU Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria,Mary Makondo ameipongeza  Ofisi ya  wakili mkuu wa  Serikali  kwa kuisaidia serikali kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa weledi na kufanikiwa kuokoa mali na fedha zaidi ya Sh.10  Trilioni tangu ofisi hiyo ianzishwe mwaka 2018.


Akizungumza  jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya mawakili  wa serikali,  yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali,Makondo amesema mafunzo hayo ya siku nne,anaamini yatawajengea uwezo zaidi wa kuisimamia serikali katika utekelezaji  wa miradi mikubwa na ya kimkakati.


“Nawapongeza sana kusaidia serikali katika utekelezaji wa majukumu yake na kuokoa fedha hizi toka kwenye mashauri ya madai, ambazo zimesaidia  kuendelea kutumika katika ukuaji wa uchumi wetu,nyie ni watu muhimu sana kwenye ukuaji wa uchumi wetu na uboreshaji wa pato la Taifa,”amesema.


Amesema uanzishwaji wa ofisi hiyo ulienda kuleta wabobezi,Tija na ufanisi katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi yanayofunguliwa dhidi ya serikali,ambayo kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kusaidia kuokoa fedha hizi ambazo wasingesimama kwenye weledi wao wasingeokoa na zingepotea.


“Ofisi unapaswa kuahirikiana na Taasisi zote za serikali ambazo zipo kwenye mihimili hii mitatu yaani serikali yenyewe,Bunge na Mahakama,ili kuhakikisha maslahi ya wananchi na ndani ya nchi na nje yanalindwa ipasavyo,”amesema.


Aidha, amewapongeza  kwa kuwa mstari wa mbele kutatua migogoro inayoibuka katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha maslahi ya nchi inalindwa.


Amewataka kujiandaa ipasavyo katika kupata elimu na stadi ya utatuzi wa migogoro, kwa njia ya maridhiano,majadiliano na suluhisho inayoibuka kwenye Taasisi za ndani na nje ya nchi.


“Tumeshuhudia migogoro hii imekuwa ikiongezeka na nyie watu muhimu na serikali inatambua  mchango wenu mkubwa na wengine mnahusika kutoa ushahidi,uandaaji wa nyaraka na katika uendeshaji wa mashauri hayo,iwapo mtaandaa vizuri nyaraka pamoja nakutoa ushauri itasaidia serikali kuiepusha na ulipaji wa fidia kwa wadau,”amesema.


Naye Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata amesema Ofisi yake imeshiriki kikamilifu katika kukuza uchumi ikiwemo kushiriki  kwenye utatuzi wa migogoro na mashauri  kwa wakati na kwa kushirikiana na vyombo vya utoaji haki,pamoja na kutoa ushauri kwa Mwanasheria Mkuu  na kutatua migogoro mbalimbali kwa njia ya majadiliano.


“Lakini tumeendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa weledi kwa niaba ya serikali na Taasisi zake na kuokoa fedha na mali nyingine za serikali,ambazo watu wasiostahili wangeweza kulipwa,mfano tangu kuanzishwa ofisi hii,tumeokoa zaidi ya Sh.Trilioni 10 na fedha hizi zimeendelea kutumika katika utoaji wa huduma na kukuza uchumi wa nchi,”amesema.


Malata amesema kuwa, serikali ingeshindwa mashauri hayo,basi ingewajibika kuwalipa wadai fedha hizo na kushindwa kutoa huduma na kukuza uchumi kwa kutumia fedha hizo.


Amesema  kuwa,pamoja na mafanikio hayo wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi wenye stadi maalumu (Specialized Skills) katika maeneo mtambuka kama mafuta na gesi,usuluhishi wa kimataifa,majadiliano,upungufu wa watumishi,ikama ya ofisi inataka kuwa na watumishi 312 waliopo ni 174,hivyo wana upungufu wa watumishi  138.


Pia amesema upungufu mwingine wa uhitaji  wa mafunzo kwa watumishi pamoja na vitendo kazi, ikiwa ni pamoja na vifaa vya TEHAMA pamoja na maboresho ya mifumo na miundombinu ya TEHAMA, kutopata fursa za ufadhili  wa mafunzo maalum nje ya nchi hasa katika maeneo yanayogusa mikataba inayoingiwa na serikali, ambapo utatuzi wake wa migogoro unapaswa kufanyika nje ya nchi.


Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: