Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (Mb) leo Februari 15, 2022 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara na ofisi za Tume ya Nguvu za Atomiki Kanda ya Kati iliyopo Kikombo Jijini Dodoma.


Akizungumza kabla ya uwekaji wa jiwe hilo la msingi Waziri huyo amesema ofisi hizo zitajengwa nchi nzima ikiwa ni jitihada za Serikali kusogeza huduma za mionzi karibu na wananchi na kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kutaka kurahisisha mazingira ya biashara kwa kusogeza huduma karibu na wananchi.


Profesa Mkenda amesema ili kujenga mazingira mazuri ya biashara ameitaka Bodi ya Tume hiyo kuangalia jinsi ya kufanya kazi zake kwa kupunguza gharama hususan  tozo  bila kuathiri ubora wa huduma.


"Tuangalie yale maeneo ambayo tunatumia thamani kama kigezo cha tozo hii inatupa shida, kwa mfano mtu anayetaka kuuza kahawa ambayo haijachakatwa tozo yake inakuwa ndogo kuliko yule aliyechakata, jambo ambalo linaua viwanda vyetu vya kuchakata bidhaa," amesisitiza Prof. Mkenda.


Aidha, Waziri huyo ameitaka Tume hiyo kuhakikisha inatenga fedha kwa ajili ya kusomesha wataalamu nje ya nchi ili kuongeza wataalamu wa mionzi nchini.


Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ilikuwa na changamoto ya maabara katika Kanda zake, jambo ambalo lilisababisha kuchelewa kutoa huduma kwa wananchi.


Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa katika kutatua changamoto Serikali kupitia TAEC iliweka mpango mkakati wa kuhakikisha maabara hizo zinajengwa ili kutoa huduma hiyo kwa viwango kama zilivyo nchi nyingine.


Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii Mhe. Abdallah Chikota (Mb) ameipongeza Wizara na Tume kwa kusogeza huduma kwa wananchi na kuahidi kuendelea kusemea Wizara Bungeni ili ipate fedha nyingi za maendeleo kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali.

Share To:

Post A Comment: