Na. Angela Msimbira  MBEYA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amesema serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.4  kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Tembela  ili kutatua  changamoto ya miundombinu ya  barabara na madaraja katika eneo hilo.


 Akikagua  miundombinu ya barabara katika kata ya ya Tembela , Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mkoani Mbeya  leo tarehe 15 Februari,2022  amesema  ujenzi wa Daraja la Tembela  litasaidia   kuunganisha wananchi wa Kata ya Mwasanga, Mwakibete, Tembela na Mbeya vijijini ambao walikuwa wakipata adha ya Mawasiliano ya barabara tangu daraja hilo lilipobomoka  mwaka 2019 na kusababisha vifo vya watu watano katika eneo hilo.


Waziri Bashungwa  amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha hizo na kusikiliza kilio cha wananchi wa kata hizo  ili kutoa nafuu ya mawasiliano ya barabara  katika eneo la Mbeya Mjini na Vijijini.


Amemuagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Mbeya Mhandisi Charles Mwita kuhakikisha Mkandarasi anaanza ujenzi wa Daraja hilo ifikiapo Tarehe 1 Machi, 2022 na kuhakikisha anatuma picha mnato na video zinazoonyesha ujenzi huo umeanza kufanyika.


Waziri Bashungwa amemuagiza Meneja huyo kuhakikisha  wanasimamia kikamilifu ujenzi huo ili dhamani ya fedha zilizotolewa na serikali zinatumika na kupata dhamani ya fedha iliyotolewa ziendane sambamba na ubora wa ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.


Amesema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha inatatua changamoto za miundombinu ya barabara kwa wakati na kurejesha mawasiliano katika kata husika ili kuinua uchumi  wa kata hizo.


Aidha amewashukuru wananchi  kwa kuendelea kuunga mkono serikali kwa kujitolea kuweka madaraja  mbadala lengo likiwa ni  kuhakikisha madaraja hayo yanapitika  na wananchi wanaendelea kupata huduma.


Naye Diwani kata ya  Tembela Fred Kibeso Mwasoke amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambalo linaunganisha maeneo ya Mwasanga, Mwakibete, Matembele na vijiji vinavyozunguka, kwa kuwa wanaamini kuwa uchumi utafunguka.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: