Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk John Pima amekiri kukodisha madarasa mawili katika shule binafsi ya Sojema kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi.

Amesema fedha za Mpango wa Maendeleo na Mapambano dhidi ya Covid-19 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan takribani Sh bilioni 2.1 zilikuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari tu.

Akizungumza mjini hapa jana, Pima alisema fedha hizo zilikuwa hazihusiani na ujenzi wa madarasa ya shule za msingi katika Jiji la Arusha.

Mkurugenzi alisema hayo kutokana na sintofahamu iliyokumba Halmashauri ya Jiji la Arusha, ambapo baadhi ya madiwani wanamtuhumu kutumia fedha za Covid-19 kinyume na makusudio.

Madiwani hao wamedai kuwa, Mkurugenzi huyo ameshindwa kujenga madarasa kwa ajili ya wanafunzi 1,300 kwa fedha za ndani na mapambano dhidi ya Covid-19 na badala yake amekodisha madarasa katika shule binafsi ya Sojema iliyopo Kata ya Muriet ndani ya Jiji la Arusha kwa gharama ya Sh milioni nne kwa mwaka.

Wamedai Mkurugenzi huyo amefanya hivyo bila kushirikisha Kamati ya Fedha na Uchumi, Baraza la Madiwani wala Kamati ya Ushauri Kata ya Muriet, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu.

 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita alisema wanafunzi wa darasa la kwanza wapatao 900 na wanafunzi madarasa ya awali 400 wanasoma katika madarasa ya kukodisha kwenye shule hiyo binafsi.

 Doita ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Madiwani ya Elimu, Afya na Uchumi, alisema Jiji la Arusha halijajenga hata darasa moja la shule ya msingi kwa fedha hizo mwaka jana.

Alisema Jiji la Arusha lilipitisha bajeti ya ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari kiasi cha Sh bilioni tatu na zilipitishwa katika vikao husika, lakini wanashindwa kuelewa fedha za Covid -19 Sh bilioni 2.1 zimekwenda wapi na zile zilizopitishwa zimefanya kazi gani.

Diwani wa Kata ya Muriet, Francis Mbise alikiri kukodishwa madarasa mawili katika shule ya Sojema, lakini  hajui chochote juu ya mkataba uliopo kati ya jiji na shule hiyo.

Akijibu tuhuma hizo, Dk Pima alisema aliamua kukodisha madarasa mawili katika shule binafsi kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya msingi na kwamba alishirikisha vikao husika ikiwamo Kamati ya Fedha, Uchumi na Uongozi na hakukuwa na umuhimu kushirikisha Baraza la Madiwani wala Kamati ya Ushauri ya Kata ya Muriet.

''Ni kweli tumekodisha vyumba vya madarasa katika shule binafsi ya Sojema na tumefanya hivyo ili kuondoa msongamano wa wanafunzi katika Kata ya Muriet na hiyo inatokana na mwamko wa wazazi kupeleka watoto katika shule za serikali,” alisema.

 Dk Pima alisema halmashauri imetenga Sh milioni 100 kwa ajili ya kujenga shule ya msingi katika viwanja vya PSSSF kwenye kata hiyo.

“Siwezi kufanya maamuzi kinyume cha maagizo kwa fedha za Covid-19 kwani zimeelekezwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari na tayari madarasa 105 yamejengwa,” alisema. 

Alisema madarasa nane ya shule za msingi yamejengwa katika Kata ya Muriet kutokana na vyanzo vya mapato ya ndani na kwamba kata hiyo ina shule za msingi tatu tofauti na kata nyingine yoyote ndani ya Jiji la Arusha.

Share To:

Post A Comment: