Mwandishi wetu,Arusha 


Mahakama ya mwanzo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha imemhukumu,Musa Olenaing'ure kwa kosa la kumghasi na kumbugudhi,Noondomonoki  Sabore ambaye ni mama mkwe wake.


Mahakama hiyo imemtia hatiani Olenaing'ure  chini ya kanuni ya 37 ya kanuni   za uendeshaji wa mashauri ya jinai katika mahakama za mwanzo nyongeza ya tatu ya mahakama za mahakimu   sura ya 11 rejeo la mwaka 2019.


 Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi wa mahakama hiyo,Cleophas Ndyegura alisema kuwa mahakama hiyo imejiridhisha kutokana na ushahidi kwamba mshtakiwa  aliingia kwenye nyumba ya mlalamikaji mnamo Desemba 8 mwaka Jana majira ya saa 8:00 asubuhi na kisha kumbugudhi  kinyume na sheria.


"Mahakama hii imejiridhisha kutokana na ushahidi uliotolewa kwamba ni kweli mshtakiwa aliingia kwenye nyumba hiyo kwa  lengo kumghasi au kumbugudhi mlalamikaji kwa kuwa kwenye utetezi wake alidai hakuwepo eneo la tukio siku ya tukio" alisema hakimu 


 Hakimu Ndyegura aliimbia mahakama hiyo kwamba  mahakama ilijaribu kupima ushahidi wa mlalamikaji na utetezi wa mshtakiwa na kujiridhisha kwamba  utetezi kwamba mshtakiwa hakuwepo siku ya tukio ni utetezi wenye nguvu kisheria lakini utetezi huo unatakiwa kuwa na uthibitisho kuwa ni kweli mshtakiwa hakuwepo eneo la tukio siku kosa linatendeka jambo ambalo hakutekeleza.


Hatahivyo ,hakimu Ndyegura aliiambia mahakama hiyo kwamba  kutokana na shufaa za mshtakiwa kwamba ana familia inamtegemea na ni mwajiriwa kwenye kampuni  na kwa kuzingatia ni mkosaji kwa Mara ya kwanza basi mahakama hiyo inamhukumu kifungo cha miezi mitatu jela.


Akimalizia kusoma hukumu hiyo hakimu Ndyegura alieleza kwamba  haki ya kukata rufaa kwenda mahakama ya wilaya ipo wazi kwa ambaye hajaridhika na uamuzi ndani ya siku 30 kutoka tarehe uamuzi.


Akizungumza Mara baada ya hukumu hiyo,Lasaru Ole Sabore ambaye ni baba mkwe wa mshtakiwa alisema kwamba hajaridhika na hukumu hiyo kwa kuwa haielezi mshtakiwa alienda kwenye nyumba ya mlalamikaji.


"Kuna mkanganyiko mkubwa sana ukisoma hukumu hiyo  inaeleza  siku ya tukio mshtakiwa alifika nyumbani kwake eneo la  kitongoji cha madukani na kusukuma mlango wake na kisha kuingia ndani kwake na  sio kwa mlalamikaji" alieleza Ole Sabore 


Ole Sabore alisema watakata rufaa  dhidi ya hukumu  hiyo  kwa kuwa mshtakiwa hakupewa nafasi ya kuleta ushahidi wake mahakamani na akadai anahisi huenda kuna  harufu ya rushwa katika kesi hiyo.


Hatahivyo,Leiyan Daph ambaye  ni mtoto wa mlalamikaji alieleza kwa upande wao kwamba mama yake alishinda kesi ya awali iliyohusu mgogoro wa nyumba na wanachoweza kukifanya wanaolalamikia hiyo hukumu ni kukata rufaa.


"mama yangu alishinda kesi ya awali ya kumtoa kwenye nyumba huyo mshtakiwa wao wanachoweza kufanya ni kukata rufaa tu" alisema Daph 

Share To:

Post A Comment: